MANCHESTER, Uingereza
AMETANGAZA kuwa huu ni msimu wake wa mwisho kucheza Manchester City. Ni John Stone, beki wa kati wa kimataifa wa England.
Stones atakuwa amemaliza mkataba wake na kuhitimisha miaka 10 ya utumishi katika kikosi cha Man City.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, alikuwa mchezaji wa pili kusajiliwa baada ya Pep Guardiola kuajiriwa klabuni hapo mwaka 2016. Man City walitumia Pauni milioni 48 kumng’oa Everton.
Kwa miaka yake 10, heshima yake imetokana na utulivu wake awapo na mpira, ubora wa kupiga pasi, kunusa na kuondosha hatari, pamoja na uwezo wa kusogea kwenye eneo la kiungo akitokea nyuma.
HESHIMA YAKE
Alikuwa mchezaji tegemeo wa Man City wakati timu hiyo ilipotwaa kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2022-23.

Kwa miaka yake ndani ya Etihad, Stones ameiwezesha Man City kutwaa mataji 19, yakiwamo sita ya Ligi Kuu, mawili ya FA na matano ya Kombe la Ligi.
Akiwa na mechi 87 alizoitumikia timu ya Taifa ya England, Stones ameitumikia Man City katika michezo 293.
ANGUKO LAKE
Hata hivyo, misimu miwili ya hivi karibuni haijawa mizuri kwake kutokana na majeraha, ambapo amekosa takribani mechi 60.
Majeraha hayo yamemfanya kupoteza namba katika kikosi cha kwanza, na sasa amejikuta akiwa chaguo la tano mbele ya Ruben Dias, Abdukodir Khusanov, Marc Guehi na Josko Gvardiol.
Kutokana na mazingira hayo, Stones ameona ni bora kuondoka ili kusaka timu itakayompa uhakika wa kucheza msimu ujao.
AACHA UJUMBE HUU
Lakini, Stones anaondoka akiwa anatambua mchango mkubwa wa Man City katika maisha yake ya soka. “Manchester City ina maana gani kwangu? Pamekuwa nyumbani kwa miaka 10, na patabaki kuwa nyumbani kwa kipindi chote cha maisha yangu,” amesema.
“Nilikuja hapa nikiwa mdogo na sasa naondoka nikiwa mtu mzima, baba, mume na nimetimiza ndoto nyingi nilizokuja nazo hapa.”
KURUDI EVERTON?
Bado hajaweka wazi mipango yake ya msimu ujao lakini zipo tetesi kuwa atarejea katika klabu yake ya zamani ya Everton, ambayo aliitumikia katika michezo 95, kabla ya kutua Etihad.
Everton alizoitumikia kwa miaka mitatu ilimsajili kwa Pauni milioni 3 tu akitokea Barnsley.
West Ham United nayo inatajwa kumtolea macho, kama ilivyo kwa Juventus na AC Milan na Bayern Munich inayonolewa na beki mwingine wa zamani wa Man City, Vincent Kompany.


