LOS ANGELES, Marekani
KATIKA orodha ya mastaa wenye mkwanja mrefu duniani kwa sasa, nafasi ya kwanza na ya pili zinashikwa na waongozaji wa filamu nchini Marekani, Steven Spielberg na George Lucas.
Spielberg ambaye ni ‘dairekta’ maarufu wa filamu za Marekani [Hollywood], amekuwa kwenye ubora mkubwa tangu alipochomoza katika miaka ya 1990, na sasa ana utajiri wa Dola za Marekani bilioni 7.1.
Dairekta huyo ndiye bilionea wa kwanza kutokea katika tasnia ya burudani na aliweka rekodi hiyo mwaka 1994 baada ya filamu aliyoiongoza ya Jurassic Park kufanya vizuri mwaka 1993.
Lucas ambaye naye ni dairekta na prodyuza, aliingia katika hadhi ya ubilionea mwaka 1997 na sasa anashika nafasi ya pili, nyuma ya Spielberg, katika orodha ya mastaa wenye mkwanja mrefu zaidi duniani.
Kwa upande wake, Lucas ana utajiri wa Dola bilioni 5.2. Utajiri wake uliongezeka mara dufu mwaka 2012.
Katika nafasi ya tatu, ni lejendari wa Ligi Kuu ya mchezo wa Kikapu nchini Marekani [NBA], Michael Jordan, ambaye kwa sasa utajiri wake ni Dola bilioni 4.3.
Nafasi ya nne ni Vincent McMahon, ambaye ni bosi wa mchezo wa mieleka nchini Marekani. Utajiri wake ni Dola bilioni 3.6, akifuatiwa na mtangazaji wa vipindi vya televisheni, Oprah Winfrey [Dola bilioni 3.2].
Anayefuata katika nafasi ya sita ni rapa Jay Z [Dola bilioni 2.8], Taylor Swift [Dola bilioni 2], Kim Kardashian na Peter Jackson [Dola bilioni 1.9], na mkongwe wa NBA, Magic Johnson [Dola bilioni 1.6].
Mkongwe wa mchezo wa gofu, Tiger Woods, anashika nafasi ya 11 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.5, prodyuza wa vipindi vya televisheni, Dick Wolf [Dola bilioni 1.5], na dairekta wa filamu, Tyler Perry [Dola bilioni 1.4].
Kwa upande mwingine, staa wa NBA, LeBron James, anafuata akiwa na utajiri wa [Dola bilioni 1.4], Bruce Springsteen [Dola bilioni 1.2], Arnold Schwarzenegger [Dola bilioni 1.2], na Jerry Seinfeld [Dola bilioni 1.1].
Wengine ni staa wa tenesi, Roger Federer [Dola bilioni 1.1], kama ilivyo kwa dairekta wa filamu, James Cameron, na wanamuziki Rihanna, Beyonce Knowles-Carter na Dr. Dre, ambao kwa sasa kila mmoja ana utajiri wa Dola bilioni moja.


