25.2 C
New York

Mambo 10 usiyoyajua kuhusu Kevin Keegan

Published:

LONDON, Uingereza

HIVI karibuni, tasnia ya soka duniani ilishitushwa na kifo cha lejendari wa klabu za Liverpool na Newcastle United, Kevin Keegan. Amefariki akiwa na umri wa miaka 75.

Keegan aliyecheza pia Hamburg na Southampton, aliwahi pia kuwa nahodha wa timu ya soka ya Taifa ya England, ambayo baadaye alikuja kuinoa.

BAO MECHI YA KWANZA

Liverpool chini ya kocha Bill Shankly, ilimsajili Keegan mwaka 1971 baada ya kiwango kizuri akiwa na Scunthorpe United aliyokuwa ameitumikia katika mechi zaidi ya 100.

Liverpool ilitumia Pauni 35,000 kumsajili Keegan, wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 tu, na alifunga katika mechi yake ya kwanza walipokutana na Nottingham Forest.

AACHA MATAJI SABA ANFIELD

Keegan aliondoka Anfield mwishoni mwa msimu wa 1976-77 akiwa amebeba mataji saba, yakiwamo matatu ya Ligi Kuu na mawili ya UEFA Cup (sasa Ligi ya Mabingwa) na moja la FA.

Ni baada ya Keegan kuondoka akiwa na mabao 100 katika mechi 323, ndipo Kenny Dalglish alipopata nafasi ya kuibuka, kuwika na hatimaye kuwa lejendari wa Liverpool.

ALITAKIWA MADRID, ABEBA BALLON D’OR

Alipotimka Liverpool, zilikuwepo taarifa za kutakiwa Real Madrid lakini Keegan alichagua kujiunga na Hamburg ya Ligi Kuu nchini Ujerumani (Bundesliga).

Akiwa huko, aliiongoza klabu hiyo kuwa mabingwa wa Bundesliga msimu wa 1978-79. Walikaribia kutwaa taji la Ulaya msimu uliofuata lakini walifungwa na Nottingham Forest katika mechi ya fainali.

Keegan alithibitisha ubora wake alipotwaa mara mbili mfululizo tuzo maarufu ya Ballon d’Or, akifanya hivyo mwaka 1978 na 1979.

MAISHA YA MUZIKI

Nje ya soka, Keegan alipenda muziki na alirekodi nyimbo zilizopata umaarufu tangu akiwa mchezaji katika klabu ya Liverpool.

Wakati fulani akiwa Ujerumani aliachia ngoma kadhaa, zikiwamo ‘Head Over Heels In Love’ ulioshika nafasi ya 10 katika chati za muziki nchini humo.

ARUDI ‘KUKIWASHA’ ENGLAND

Keegan alirudi katika soka la England mwaka 1980, safari hii akijiunga na kikosi cha Southampton kilichokuwa na ‘mafundi’ Alan Ball na Mike Channon.

Licha ya kutotwaa ubingwa wa Ligi, Keegan aliweza kubeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (1982) wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa nchini humo.

NAHODHA TIMU YA TAIFA

Keegan aliannza kuitumikia timu ya soka ya Taifa ya England ‘Three Lions’ mwaka 1974, kisha kupanda hadi kuwa nahodha wa kikosi.

Baada ya miaka 10 ya kufanya kazi na England, alistaafu akiwa amecheza mechi 63 (31 akiwa nahodha) na kufunga mabao 21.

AIPANDISHA DARAJA NEWCASTLE

Kuelekea msimu wa 1982-83, Newcastle United ilimng’oa Southampton kwa ada ya Pauni 100,000.

Keegan, kama kawaida yake, alifunga bao katika mechi yake ya kwanza (dhidi ya QPR), wakati huo Newcastle ikiwa Daraja la Kwanza.

Msimu uliofuata, Newcastle ilifanikiwa kupanda Daraja na kutinga Ligi Kuu. Hata hivyo, Keegan alitangaza kuwa angestaafu mwishoni mwa msimu huo wa 1983-84.

AIOKOA NEWCASTLE AKIWA KOCHA

Miaka nane baada ya kustaafu na kwenda kuishi na familia yake nchini Hispania, Keegan alirudi Newcastle, safari hii akiwa kocha na timu hiyo ikiwa imerudi Daraja la Kwanza.

Akiwa kocha, Newcastle ikarejea Ligi Kuu. Katika msimu wa 1993-94, ikamaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, nyuma ya mabingwa Man United na Blackburn Rovers.

Keegan alitangaza kujiuzulu kuinoa Newcastle mwaka 1997, akisema anahisi amefanya vya kutosha kuisadia klabu hiyo.

Alipoondoka Newcastle, Keegan aliibukia Fulham akiwa kama ofisa uendeshaji, kabla ya kupewa benchi la ufundi na kuisadia kurudi Ligi Kuu.

APEWA BENCHI ‘THREE LIONS’

Ni baada ya Fulham, ndipo alipoajiriwa kuliongoza benchi la ufundi la timu ya soka ya Taifa ya England mwaka 1999 akichukua nafasi ya Glenn Hoddle.

Aliiwezesha ‘Three Lions’ kufuzu fainali za EURO 2000 lakini timu yake hiyo iliishia hatua ya makundi baada ya kushinda moja katika mechi tatu.

Akiendelea kukosolewa kwa kiwango kibovu na matokeo yasiyoridhisha, Keegan alijizulu wakati wa mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002.

AIPANDISHA DARAJA MAN CITY

Mwaka 2001, Keegan aliajiriwa Manchester City kuchukua nafasi ya kocha Joe Roy. Aliweza kuipandisha Ligi Kuu ikiwa mabingwa wa Daraja la Kwanza.

Akiwa amemuongeza kikosini Nicolas Anelka, Man City ilimaliza msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo.

Aliondoka klabuni hapo Machi, 2005, na iliwashangaza wengi kuona anarudi Newcastle, ambako nako alidumu kwa miezi nane tu, kisha akaachana kabisa na mchezo wa soka.

Related articles

Recent articles