CALIFORNIA, Marekani
FAINALI za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) zimeshuhudia historia nyingi zikiandikwa lakini moja ya hizo ni uwepo wa Dk. Suzanne Huurman.
Katika mabenchi ya timu zote 48 zinazoshiriki michuano ya msimu huu, Dk. Suzanne ndiye mwanamke pekee ambaye ni Mkuu wa idara ya tiba.
Dk. Suzanne ni Mkuu wa Idara ya tiba kwa upande wa Curacao, wakati timu zingine 47 zikiwa na wanaume kwenye nafasi hiyo.
Mzaliwa huyo wa Brazil amewahi kufanya kazi akiwa daktari katika klabu za Real Madrid na PSV, pia akihudumu kwenye U-16 ya Uholanzi kwa upande wa timu ya mpira wa mikono.
Katika msafara wa watu 49 wa Curacao uliosafiri kwenda Kombe la Dunia msimu huu, Dk. Suzanne alikuwa mwanamke pekee.
Mtaalamu huyo wa sayansi ya michezo, anafichua changamoto kubwa iliyopo kwa madaktari wa kike kufanya kazi katika soka, mchezo uliotawaliwa na wanaume kwa kiasi kikubwa.
“Kama una familia au ujauzito, utakuwa nje ya timu kwa muda. Hivyo, huwezi kuedana na ratiba ya msimu wa soka.
“Lazima apatikane mtu wa kuchukua nafasi yako. Ni ngumu kwa sababu unatakiwa kupatikana kwa ajili ya timu,” amesema.


