LONDON, Uingereza
KUELEKEA fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni 11, 2026, umekuwapo wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi viwanjani.
Michuano hiyo itafanyika katika nchi tatu, ikiwamo Marekani, ambayo kwa miaka michache ya hivi karibuni imekuwa kwenye uhusiano mbaya wa kimataifa.
Mathalan, kwa sasa Marekani iko kwenye mapigano na Iran, ambayo inaungwa mkono na makundi makubwa ya kigaidi huko Mashariki ya Kati, likiwamo la Hezbollah nchini Lebanon na Hamas nchini Palestina.
Je, vikundi hivyo vinaweza kutumia fainali za Kombe la Dunia kuonesha nguvu na jeuri ya kwa Marekani na washirika wake, hasa Israel?
Hofu hiyo inatokana na taarifa kwamba mashambulizi ya Marekani na Israel yameshaua viongozi zaidi ya 250 wa Iran, hivyo huenda Taifa hilo la Kiarabu likaamua kutumia fainali za Kombe la Dunia kulipiza kisasi.
Kwa upande mwingine, fainali za Kombe la Dunia zinakuja wakati ambao Marekani iko kwenye uhusiano mbaya na wapiganaji wa Iraq, Kataib Hezbollah, baada ya kumkamata na kumshikilia kiongozi wao, Mohammad Baqer Saad Dawood al-Saadi.
Mexico, ambako pia zitachezwa baadhi ya mechi, nako kuna tishio kubwa la usalama kutokana na uwepo wa magenge makubwa ya uhalifu wa dawa za kulevya, mengi yakitajwa na Marekani kuwa ni ‘makundi ya kigaidi’.
Februari, 2026, ni kama Serikali ya Mexico ilitangaza vita na genge maarufu la Jalisco New Generation Cartel baada ya kumuua kiongozi wao, Nemesio Ruben Oseguera Cervantes ‘El Mencho’.
Hatua hiyo inaibua hofu juu ya hatua wananyoweza kuchukua ‘wahuni’ hao katika mechi 12 za Kombe la Dunia zitakazochezwa Kusini mwa Mexico.
Wakati huo huo, historia inaonesha na kukumbusha pia, kwamba magaidi wametumia mara kadha majukwaa makubwa ya michezo duniani kuonesha jeuri yao. Mifano iko mingi.
Wakati wa michuano ya Olimpiki ya mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani, shambulizi lililotekelezwa na magaidi wa Palestina lilisababisha vifo vya wanamichezo tisa wa Israel.
Mwaka 1998, wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa, magaidi wa Algeria walipanga kulipua bomu katika baadhi ya mechi.
Ni kama ilivyokuwa mwaka 2015, wakati wa mechi kati ya Ufaransa na Ujerumani, ambapo lilikuwapo jaribio la kutegwa bomu kwenye Uwanja wa Stade de France.


