28.1 C
New York

Makocha hawa ‘out’ baada ya Kombe la Dunia 2026

Published:

LONDON, Uingereza

NI siku 10 tu zimebaki kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Wakati Argentina ikienda kama bingwa mtetezi, Brazil ambao ni wapinzani wao wakubwa kwa Bara la Amerika ya Kusini, ndiyo bingwa mara nyingi (5) katika historia ya michuano hiyo.

Kwa upande mwingine, huenda fainali hizo za kwanza kushirikisha timu 48 zikawa za mwisho kwa baadhi ya makocha.

Ndiyo, kuna makocha watano, ambao mikataba yao na timu zao itakwisha mara tu fainali za Kombe la Dunia zitakapomalizika.

DIDIER DESCHAMPS

Kocha wa timu ya Taifa ya Ufaransa. Alikuwa kwenye benchi wakati Les Bleus wakitwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Msimu uliopita, walifika fainali lakini safari hii hawakubeba ‘ndoo’ mbele ya Argentina ya akina Lionel Messi.

Deschamps, kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa, ameweka wazi kuwa huu utakuwa atajiuzulu baada ya Kombe la Dunia mwaka huu.

ZLATKO DALIC

Mkongwe huyo amekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Croatia kwa miaka tisa. Tangu alipoajiriwa mwaka 2017.

Katika fainali za mwaka 2018, Dalic aliiongoza Croatia kufika fainali ya Kombe la Dunia. Msimu uliopita, 2022, timu hiyo ilishika nafasi ya tatu.

Kwa sasa, mkataba wake na ‘Vatreni’ utafikia ukomo baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia. Huenda akachukua uamuzi wa kupumzika au kuhamia katika ngazi ya klabu.

ROBERTO MARTINEZ

Baada ya kuajiriwa mwaka 2023, aliiwezesha timu ya Taifa ya Ureno kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Nations League).

Endapo atafanya vizuri msimu huu wa Kombe la Dunia, huenda akaongezwa mkataba wa kuendelea kuinoa timu hiyo ya barani Ulaya.

Kinyume cha hapo, huenda kocha huyo wa kimataifa wa Ubelgiji akarejea katika soka la ngazi ya klabu.

RONALD KOEMAN

Safari hii, kikosi cha Uholanzi kinanolewa na kocha mzawa na mwenye uzoefu wa kutosha, Ronald Koeman.

Koeman ambaye aliwahi kufanya kazi Ligi Kuu ya England akiwa na Everton, pia wakati fulani akiinoa timu kongwe ya La Liga, Barcelona.

Koeman ana miaka mitatu kwenye benchi la Uholanzi, tangu walipompa kazi mwaka 2023. Mkataba wake na ‘Oranje’ utakwisha Julai 31, 2026.

MAURICIO POCHETTINO

Muargentina huyo amekuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Marekani kwa miaka miwili tangu alipoajiriwa mwaka 2024.

Hajaipa timu hiyo taji lolote kubwa na mkataba wake na Marekani utafikia ukomo baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia.

Pochettino aliyewahi kufanya kazi Tottenham, PSG na Chelsea, anahusishwa na AC Milan, ambayo hivi karibuni iliachana na kocha Massimiliano Allegri.

Related articles

Recent articles