NYON, Uswis
HIVI unafahamu kuwa zimeshafungwa ‘hat-trick’ 54 katika historia ya michuano ya soka ya Kombe la Dunia kwa wanaume tangu ilipoanza mwaka 1930?
Chukua hiyo. Sasa, makala haya yanakuibulia mambo usiyoyajua kuhusu ‘hat-trick’ hizo zilizofungwa kwa nyakati tofauti.
Mosi, hadi leo hii, hakuna mchezaji aliyefunga ‘hat-trick’ mbili za mchezo mmoja. Oleg Salenko wa Urusi alikaribia kuweka rekodi hiyo mwaka 1994 lakini alifunga mabao matano katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Cameroon.
Pili, rekodi ya ‘hat-trick’ ya mapema zaidi ya Kombe la Dunia inashikiliwa Laszlo Kiss wa Hungary, ambaye alitumia dakika saba tu kufunga mara tatu katika mchezo dhidi ya El Salvador mwaka 1982.
Tatu, mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga ‘hat-trick’ ni Pele wa Brazil. Alifanya hivyo mwaka 1958 akiwa na miaka 17 na siku 244 katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Ufaransa.
Nne, Cristiano Ronalo ndiye mchezaji ‘mzee’ zaidi kufunga ‘hat-trick’. Mreno huyo alifanya hivyo dhidi ya Hispania akiwa na umri wa miaka 33 na siku 130, mchezo huo ukimalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Tano, katika historia ya Kombe la Dunia, kuna wachezaji wanne tu waliowahi kufunga ‘hat-trick’ lakini timu zao zikaishia kufungwa. Nyota hao ni Ernst Wilimowski (Poland), Josef Hugi (Uswis), Igor Belanov (USSR, sasa ikiitwa Urusi) na Kylian Mbappe (Ufaransa).
Sita, Gabriel Batistuta alistaafu akiwa amefunga ‘hat-trick’ mbili (1994 na 1998). Cha kushangaza, zote alifunga Juni 21, dhidi ya timu zinazoshiriki kwa mara ya kwanza, na mabao yote ya mwisho yalitokana na penalti.
Saba, fainali pekee za Kombe la Dunia ambazo hazikuwa na ‘hat-trick’ hata moja ni zile za mwaka 2006 zilizofanyika katika ardhi ya Ujerumani.
Nane, kati ya ‘hat-trick’ 54 zilizopo kwenye historia ya Kombe la Dunia, 23 zilifungwa katika mechi zilizochezwa Jumapili.
Mwisho, Geoff Hurst wa England ndiye mchezaji wa kwanza kufunga ‘hat-trick’ katika mchezo wa fainali. Alifanya hivyo mwaka 1996 walipoifunga Ujerumani ya Magharibi mabao 4-2. Mbappe alifanya hivyo mwaka 2022.


