Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza zaidi ya tani nne za dawa za kulevya zilizokuwa zikihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyoko mahakamani, katika hatua inayoashiria dhamira ya Serikali kudhibiti biashara haramu ya dawa hizo nchini.
Zoezi hilo limefanyika, Oktoba 3, 2025, katika kiwanda cha saruji cha Twiga Cement, kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam, likiongozwa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ambaye ametangaza msamaha maalum kwa wauzaji wa dawa hizo watakaoamua kujisalimisha kwa hiari.
“Wapo wengi, mapapa wa dawa za kulevya, wengine wamekimbilia nchi mbalimbali za Afrika na hata nje ya bara. Tunaendelea kuwafuatilia katika nchi walizokimbilia ili mkono wa sheria uwafikie,” amesem Lyimo.
Aidha, alitoa wito kwa wote wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja na kujisalimisha, akibainisha kuwa Mamlaka haitowachukulia hatua za kisheria watakaoamua kuachana na biashara hiyo na kushirikiana na vyombo vya dola katika mapambano hayo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema jumla ya kilogramu 4,402.02 za dawa za kulevya — sawa na zaidi ya tani nne — zimeteketezwa leo kwa mujibu wa sheria.
Alifafanua kuwa dawa zilizoteketezwa ni pamoja na:
- Methamphetamine: kilogramu 2,168.18
- Heroin: kilogramu 1,064.29
- Cocaine: gramu 326.95
- Bangi: kilogramu 515.48
- Mirungi: kilogramu 653.74
Amesema dawa hizo zilikuwa sehemu ya vielelezo vya mashauri yaliyoko mahakamani, ambapo baadhi ya kesi bado zinasikilizwa, huku nyingine zikiwa zimekwishatolewa hukumu.
“Kwa mashauri ambayo bado hayajakamilika, mahakama iliagiza dawa hizo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo,” amesema Lyimo, akibainisha kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, ambayo inataka vielelezo hivyo kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa.
Miongoni mwa mashauri yaliyohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed, iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29.
Katika mashauri yaliyohitimishwa kwa hukumu, Kamishna Lyimo alitaja majina ya waliopatikana na hatia kuwa ni Hassan Azizi, Salum Shaaban Mpangula, na Hemed Juma Mrisho (Hororo) — wote hao wamelipwa kifungo cha maisha jela.
Wengine ni Ramadhan Shaban Gumbo (miaka 30 jela), Irene Dickson Mseluka (miaka 5 jela) na Gema Victor Mmasy (miaka 3 jela).
Kamishna Lyimo amesisitiza kuwa DCEA itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria na kiutendaji ili kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya, ambazo zimekuwa zikiathiri jamii, hasa vijana.
“Sambamba na hatua hizo, Mamlaka itaendelea kuutaarifu umma kuhusu taarifa zinazohusu dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano na wananchi katika mapambano haya,” aliongeza.
Kwa mujibu wa DCEA, uteketezaji wa dawa hizo ni sehemu ya mikakati endelevu ya Serikali kuhakikisha vielelezo vinavyohusiana na dawa za kulevya havitumiki tena kinyume cha sheria, sambamba na kudhibiti mzunguko wa dawa hizo hatarishi nchini.


