3.6 C
New York

Utafiti: Kukosa usingizi chanzo ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

KUKOSA muda wa kutosha wa kulala, hasa nyakati za usiku, kunaweza kusababisha ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, kwa mujibu wa utafiti mpya nchini Marekani.

Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na watafiti hao, watu wanaokosa muda wa kulala vizuri walau siku tatu kwa wiki wako hatarini zaidi kwa asilimia 40 kupata changamoto hiyo. Akizungumzia matokeo ya utafiti wao, Dk. Diego Carvalho, ambaye ni mtaalamu wa dawa za usingizi kutoka Taasisi ya American Academy, anasema:

“Kukosa usingizi hakuishii kukupa tabu siku inayofuata, bali pia huathiri uwezo wa ubongo kutunza kumbukumbu hapo baadaye.”

Utafiti huo uliofanyika kwa miaka mitano na kuchapishwa katika jarida maarufu la masuala ya afya la Neurology, ulihusisha watu 2,750 wenye wastani wa umri wa miaka 70. Kati ya watu hao, 440 walibainika kuwa na changamoto ya kukosa usingizi na asilimia zaidi ya 40 walionekana pia kuwa na uwezo mdogo wa kuhifadhi kumbukumbu ya matukio mbalimbali.

Aidha, watafiti walibaini kuwa kukosa usingizi kunaathiri tishu za ubongo zinazofahamika kwa jina la ‘hyperintensities’, ambazo huhusika katika uhifadhi wa kumbukumbu.

“Lakini pia, vipimo vyetu vimeonesha kuwa kukosa usingizi kunaathiri moja kwa moja mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo. Hivyo basi, naweza kusema majibu ya utafiti wetu yanathibitisha kuwa usingizi si tu kwa ajili ya kupumzisha mwili, bali pia huimarisha ufanisi wa ubongo,” anasema Dk. Carvalho.

Kwa upande wake, utafiti huo unakuja wakati ukiwepo mwingine wa mwaka jana ulioonesha kuwa katika watu sita nchini Uingereza, mmoja anakabiliwa na changamoto ya kukosa usingizi.

Lakini pia, mbali ya kupoteza kumbukumbu, pia kukosa usingizi huweza kusababisha magonjwa mbalimbali, ikiwamo saratani na kupooza. Wakati huo huo, watu takribani 900,000 nchini humo wanateswa na tatizo la kupoteza kumbukumbu, idadi ikitarajiwa kufikia milioni 1.7 miaka 20 ijayo, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha London.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img