RIYADH, Saudi Arabia
STAA wa soka, Cristiano Ronaldo, ameingia kwenye historia nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 100 akiwa na klabu nne tofauti.
Hata hivyo, ‘CR7’ ameweka rekodi hiyo, licha ya kikosi chake cha Al Nassr kukosa taji la Saudi Super Cup baada ya kufungwa na Al-Ahli.
Mchezo huo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Hong Kong, China, ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, kabla ya Al-Ahli kupata ushindi kwa penalti 5-3.
Ronaldo alifunga bao la kwanza, hivyo kufikisha mabao 40 tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Saudi Arabia mwishoni mwa mwaka 2022.
Alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti ya dakika ya 41, kabla ya kiungo wa zamani wa Barcelona, Franck Kessie, kuisawazishia Al-Ahli.
Akiwa Real Madrid, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno alipachika mabao 450, kisha 145 alipokuwa Manchester United, wakati huo akiwa na 101 pale Juventus.
Kwa upande mwingine, Ronaldo ambaye hajatwaa taji kubwa lolote tangu atue Saudi Arabia, bado ndiye mchezaji pekee duniani mwenye mabao mengi (138) akiwa na timu ya taifa.
Published:


