MANCHESTER, Uingereza
BEKI wa Manchester City, Ruben Dias, ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya jijini Manchester.
Diaz, raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 28, alikuwa amebakiza miaka miwili, hivyo sasa atabaki Etihad hadi mwaka 2029.
Nyota huyo alijiunga na Man City mwaka 2020 akitokea Benfica, usajili wake ukigharimu kiasi cha Pauni milioni 65.
Katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo, Diaz alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Kwa miaka yake mitano akiwa mchezaji wa Man City, ametwaa mataji saba, yakiwamo manne ya EPL na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kusaini mkataba mpya, alisema: “Nimefurahi sana. Nalipenda Jiji la Manchester, ni kama nyumbani sasa. Nawapenda mashabiki wa Manchester City.”
Kumalizana na Diaz kunawafanya mabosi wa Man City sasa kuwageukia John Stones, Ilkay Gundogan, Ederson na Bernardo Silva, ambao wamebakiza mwaka mmoja kila mmoja.
Published:


