11.6 C
New York

Eberechi Eze; Silaha nyingine mpya ndani ya Emirates

Published:

LONDON, England
ARSENAL hawatanii. Wakati mabosi wa Tottenham wakiamini ni suala la muda kumtambulisha, Arsenal waliingilia na kumalizana na mshambuliaji wa Crystal Palace, Eberechi Eze. Arsenal wameinasa saini ya nyota huyo wa kimataifa wa England kwa ada ya Pauni milioni 60.
Ifahamike kuwa Washika Bunduki wa Kaskazini mwa Jiji la London wamevunja mkataba wake uliobakiza miaka miwili. Taarifa zinaeleza kuwa Eze alivutiwa zaidi na Arsenal, ambayo iliwahi kuwa naye miaka mingi iliyopita, wakati huo akiwa kinda wa ‘academy’ yao.
Ndiyo, historia inaonesha kuwa alianza soka akiwa Arsenal, kabla ya kuondoka akiwa na umri wa miaka 13 na kujiunga na Fulham na baadaye Reading.
KWANINI ARTETA AMEMSAJILI?
Msimu uliopita, Eze mwenye umri wa miaka 27 aliifungia Palace jumla ya mabao 14, likiwamo la ushindi wa 1-0 katika fainali ya FA dhidi ya Manchester City.
Uamuzi wa Mikel Arteta kumgeukia Eze ulitokana na wasiwasi wake kwa Kai Havertz, ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti.
AMEACHA KILIO TOTTENHAM
Eze ambaye ni binamu wa mwigizaji maarufu wa Marekani, Ego Nwodim, alijiunga na Palace mwaka 2020 akitokea Queens Park Rangers, usajili huo ukigharimu kitita cha Pauni milioni 19.5.
Palace walivutiwa na kiwango kilichompa Eze tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa QPR, akiibeba mara mbili klabuni hapo.
QPR imekuwa ikivuna asilimia 15 ya mauzo ya Eze, ikiwamo hii ya sasa anapojiunga na Washika Bunduki wa Kaskazini mwa Jiji la London.
Kwa upande mwingine, Tottenham kumkosa Eze ni pigo kwao msimu huu, endapo hawataingia sokoni kusaka mchezaji wa aina yake. Kocha mpya, Thomas Frank, aliihitaji huduma ya Eze baada ya kuona James Maddison kupata majeraha.
NAFASI YAKE KIKOSINI
Ni wazi kuwa usajili wa Eze umelenga kulipa makali eneo hilo la kiungo wa pembeni wa kushoto.
Kwa miezi takribani 18, Arsenal imekuwa na changamoto katika eneo hilo. Gabriel Martinelli na Leandro Trossard wameshindwa kuwa kwenye ubora wa kumtuliza kocha wao.
Licha ya ujio wa Noni Madueke mwenye umri wa miaka 23, Eze ni mzoefu zaidi. Wakati huu Riccardo Calafiori akiwa kwenye kiwango bora akitokea beki wa kushoto, itakuwa ni nafasi nzuri kwa Eze kusaidiana naye katika eneo hilo.
Katika mfumo wa 4-3-3, huenda kikosi cha kwanza cha Arsenal kikawa na mwonekano huu; Raya, Timber, Saliba, Gabriel, Calafiori, Odegaard, Zubimendi, Rice, Saka, Gyokeres na Eze. Pia, huenda atacheza kiungo wa kati. Asilimia kubwa ya mechi alizocheza kwa kiwango cha juu akiwa Palace, alitumika katika eneo la kiungo wa kati (namba 8), ambapo anakuwa huru zaidi kuchezea mpira.
Katika mechi ambazo Arteta anataka kumiliki mchezo, anaweza kumtumia Eze na Martin Odegaard. Ni nafasi ambayo amekuwa akiwatumia Declan Rice au Mikel Merino.
Katika majukumu hayo, Arteta atakuwa na mfumo wa 4-3-3 na ‘first eleven’ yenye mwonekano huu; Raya, Timber, Saliba, Gabriel, Calafiori, Odegaard, Zubimendi, Eze, Saka, Gyokeres na Martinelli.
‘CV’ YAKE KIMATAIFA
Enze angeweza kuiwakilisha Nigeria katika soka la kimataifa kwani ndiko wanakotokea wazazi wake.
Lakini, Enze alichagua England na alianza kuitwa kikosini mwaka 2021, wakati kocha Gareth Southgate alipoita wachezaji 33 kuelekea fainali za Euro 2020.
Hata hivyo, aliumia siku hiyo hiyo akiwa mazoezini. Mwaka 2023, Southgate alimwita tena na kucheza mechi yake ya kwanza Juni 16.
Aliingia dakika ya 70 akichukua nafasi ya James Maddison katika mchezo wa kufuzu Euro 2024, ambapo England iliifunga Malta mabao 4–0.
Aliingia kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza Juni 3, mwaka jana, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Bosnia, ambapo alicheza dakika 63 na kumpisha Jack Grealish.
Machi 24, mwaka huu, ndipo Eze alipofunga bao lake la kwanza akiwa na ‘uzi’ wa England, mchezo walioshinda mabao 3–0 dhidi ya Latvia.
Kwa sasa, anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa pili wa Palace kuifungia bao timu ya taifa ya England, baada ya Peter Taylor kufanya hivyo mwaka 1976.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img