LILONGWE, Malawi
KWA mara ya kwanza katika historia ya siasa za Malawi, wagombea wengi wa kiti cha urais wamewateua wanawake katika nafasi ya mgombea mweza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Ikumbukwe, wanawake ni zaidi ya asilimia 57 ya waliojiandikisha kupiga kura, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi.
Taifa hilo la Kusini mwa Afrika lenye watu milioni 2 litafanya Uchaguzi wake Septemba 16 na hatua hiyo ya wanawake kupewa nafasi ni matokeo ya jitihada kubwa za asasi za kiraia nchini humo.
Asasi hizo zimekuwa zijipigania usawa wa kijinsia, zikiendesha kampeni mbalimbali za kuhimiza asilimia 50 ya uwakilishi wa wanawake bungeni .
Hata hivyo, Sainala Kalebe, ambaye ni mhadhiri wa masomo ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Malawi, anaamini bado haitoshi kwa wanawake kupewa nafasi ya mgombea mwenza, na badala yake vyama vyao viwaamini kuviwakilisha katika kiti cha urais.
Kalebe, katika hatua nyingine, anasema hata kwa Malawi, chama kikubwa pekee kilichothubutu kumpa mwanamke nafasi ya mgombea mwenza wa urais ni Democratic Progressive Party (DPP).
Kwa Malawi, Joyce Banda, mwanasiasa mwenye umri wa miaka 74, ndiye mwanamke pekee anayegombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mwaka 2012, Banda aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Malawi, alitokea katika nafasi ya Makamu wa Rais baada ya ‘bosi’ wake, Bingu wa Mutharika, kufariki.
Banda akilazimika kuondoka nchini humo mwaka 2014 baada ya kushindwa Uchaguzi, wakati huo akikabiliwa na shutuma za rushwa. Alirejea mwaka 2018.
Licha ya Malawi kuonesha jitihada, bado Rwanda inaongoza barani Afrika ikiwa na asilimia 61 ya uwakilishi wa wanawake bungeni, ikifuatiwa na Namibia (50%) na Senegal (46%).
Malawi ina asilimia 20 lakini imeonekana kupiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka 2019, Taifa hilo liliandika historia ya kuwa na mwanamke wa kwanza katika nafasi ya Meya kupitia kwa Juliana Kaduya.
Mwaka huo pia, Catherine Gotani Hara alitangazwa kuwa Spika wa Bunge wa kwanza mwanamke katika historia ya siasa za Malawi, nafasi anayoishikilia hadi sasa.
Mwisho, hoja ya jinsia inaweza isiwe na maana kubwa kwa Afrika, na badala yake wananchi wanahitaji viongozi watakaoshinda vita ngumu dhidi ya umasikini, rushwa, na matatizo yao kwa ujumla.
Nguvu ya wanawake Uchaguzi Mkuu Malawi
Published:


