NAIROBI, Kenya
ILE ahadi ya Rais wa Kenya, William Ruto, kuwapa kitita cha fedha katika kila ushindi imeendelea kuwatajirisha wachezaji wa Harambee Stars.
Rais Ruto aliahidi ‘mzigo’ katika kila sare au ushindi wa mechi za msimu huu wa fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Katika mechi ya ufunguzi, kila mchezaji wa Harambee Stars alilamba Shilingi milioni moja za Kenya (takribani Sh mil. 19 za Tanzania) kwa kuifunga DRC bao 1-0.
Baada ya sare katika mechi ya pili dhidi ya Angola, safari hii kila mchezaji amevuna Shilingi 500,000 za Kenya, sawa na Sh mil. 9 za Tanzania.
Kupitia taarifa yake, Wizara ya Michezo ilieleza kuwa Rais Ruto ataendelea kutimiza ahadi yake.
Achilia mbali posho hizo, Rais Ruto ameahidi kuwapatia wachezaji kiasi cha Shilingi milioni 600 za Kenya endapo watatwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Published:


