CAIRO, Misri
VIGOGO wa soka Misri, Zamalek, wamekamilisha usajili wa kiungo wa pembeni wa kimataifa wa Brazil, Juan Alvina.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, ametokea FC Oleksandriya ya Ukraine na amesaini mkataba wa miaka minne na Zamalek.
Msimu uliopita, Alvina alikuwa kwenye kiwango bora, ambapo alifunga mabao sita na kutoa ‘asisti’ tano katika mechi 24 tu za Ligi Kuu ya Ukraine.
Mchango wake kikosini uliiwezesha FC Oleksandriya kumaliza msimu ikiwa nafasi pili kwenye msimamo wa Ligi, ikizidiwa pointi tatu tu na mabingwa Dynamo Kyiv.
Zamalek imeweza kumsajili Alvina baada ya winga wake raia wa Tusinia, Ahmed Jafeli, kutua kwa mkopo katika klabu ya Abha Club ya Saudi Arabia.
Usajili wa Alvina ni mipango ya Zamalek kurudi kivingine baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Misri. Anakuwa mchezaji wa 10 kusajiliwa majira haya ya kiangazi.
Published:


