15 C
New York

Pogba na usajili wa kamari Ligue 1

Published:

PARIS, Ufaransa
ALIPOFUNGIWA kujihusisha na soka kwa miaka minne baada ya kubainika kutumia dawa za kuongeza nguvu, maswali yalikuwa mengi juu ya hatima ya kiungo raia wa Ufaransa, Paul Pogba.
Oktoba, mwaka jana, adhabu hiyo ilipunguzwa na ndipo ‘mido’ huyo wa zamani wa Manchester United na Juventus alipotakiwa kutumikia miezi 18 pekee.
Hata kabla ya adhabu hiyo, Pogba alikuwa na changamoto nyingi, ikiwamo skendo ya kukiri kwenda kwa mganga kwa lengo la kupata suluhisho la majeraha ya mara kwa mara.
Aliyasema hayo baada ya kaka yake ambaye pia ni mwanasoka, Mathias, kusema Pogba amekuwa akienda kwa waganga ili ‘kumroga’ staa mwenzake wa Ufaransa, Kylian Mbappe.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Pogba alisema matukio ya aina hiyo yalichangia kushuka kwa kiwango chake ndani ya uwanja.
Pogba mwenye umri wa miaka 32, amesaini mkataba wa miaka miwili na AS Monaco ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Pogba, ambaye hajacheza soka la ushindani tangu Septemba, 2023, pia alikuwa akihusishwa na klabu za Marekani, Saudi Arabia na Japan.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Pogba kucheza Ligue 1. Aliondoka nchini kwao, Ufaransa, kujiunga na ‘academy’ ya Man United akiwa na umri wa miaka 16.
Kwa upande mwingine, ni kama Monaco imecheza kamari kumsajili Pogba kwani klabu nyingi zilihofia kwa kuona mchezaji huyo hayuko fiti baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Katika hilo, Mkurugenzi wa Marseille, Medhi Benatia, amekiri kuwa walimtaka Pogba lakini waliachanaye naye wakihofia asingekuwa na msaada kikosini.
“Tulifikiria (kumsajili Pogba), tulitaka kumsajili,” alisema Benatia na kuongeza: “Tatizo ni kwamba kama tungemsajili Pogba, ambaye pia hayuko fiti, asingetusaidia.”
Je, Pogba atawika akiwa Ligue 1 na kuitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa? Ni swali linalosubiri majibu.
Nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa taji la Kombe la Dunia mwaka 2018. Milango iko wazi kurejea kundini endapo kiwango chake kitamshawishi kocha Didier Deschamps.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img