LONDON, Uingereza
HIVI karibuni, Liverpool walivuna kitita cha Pauni milioni 65.5 kwa kumpiga bei mshambuliaji wake, Luis Diaz, na kuingia kwenye moja ya rekodi za Ligi Kuu ya England (EPL).
Ni kwa maana hiyo basi, sasa Diaz raia wa Uruguay anaungana na mastaa wengi waliosajiliwa nje ya EPL kwa mkwanja mrefu.
PHILIPPE COUTINHO (LIVER – BARCA)
Mbrazil huyo anabaki kuwa mchezaji ghali zaidi kuondoka EPL. Alijiunga na Barca mwaka 2018 baada ya Liverpool kupokea kitita cha Pauni 115.
Baada ya kushindwa kung’ara Camp Nou, Coutinho alitimkia kwa mkopo Bayern Munich, kabla ya kwenda Aston Villa, ambako hata hivyo bado hakuweza ‘kufufua’ makali aliyokuwa nayo Anfield.
EDEN HAZARD (CHELSEA – MADRID)
Akiwa kwenye ubora mkubwa EPL, Madrid walitumia Pauni milioni 103 kumng’oa winga huyo katika kikosi cha Chelsea mwaka 2019.
Hata hivyo, akiwa Madrid, aliishia kufunga mabao saba na kutoa ‘asisti’ 12 katika mechi 76. Alivunjiwa mkataba mwaka 2023.
GARETH BALE (SPURS – MADRID)
Mwaka 2013, Madrid hawakuona hasara kutumia Pauni milioni 86 kumsajili Bale kutoka Tottenham.
Akiwa Santiago Bernabeu, atakumbukwa kwa kuvunja rekodi ya kufikisha mabao zaidi ya 100. Alistaafu mwaka 2023 akiwa Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
HARRY KANE (SPURS – BAYERN)
Baada ya kuipachikia mabao 280, nahodha huyo wa timu ya taifa ya England aliondoka Tottenham na kutua Bayern Munich kwa ada ya Pauni milioni 81 mwaka 2023.
Kane alifunga mabao 44 katika msimu wake wa kwanza Allianz Arena, licha ya Bayern kukosa taji la Bundesliga mbele ya Bayer Leverkusen.
CRISTIANO RONALDO (MAN UNITED – MADRID)
Matajiri wa La Liga, Real Madrid, walitumia Pauni milioni 80 kumng’oa Old Trafford mwaka 2009. Alisajiiwa kuziba pengo la mkongwe Raul.
Mechi 438 alizocheza zilimshuhudia Ronaldo akipachika mabao 450, kabla ya kujiunga na vigogo wa Serie A, Juventus.
Baadaye, ‘CR7’, nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, alirejea Old Trafford chini ya kocha Erik ten Hag, ambaye hata hivyo alikorofishana naye na kutimkia Al Nassr ya Saudi Arabia.
LUIS SUAREZ (LIVER – BARCA)
Aliondoka Liver mwaka 2014 kwa Pauni milioni 69.9 na kwenda kutengeneza ‘pacha’ kali na Lionel Messi na Neymar katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona.
Baada ya mabao mengi aliyofunga, pia akitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Suarez alitimkia Atletico Madrid mwaka 2020 na kubeba ‘ndoo’ ya La Liga msimu wa 2020-21.
LUIS DIAZ (LIVER – BAYERN)
Winga huyo wa kimataifa wa Colombia alisajiiwa na Liverpool mwaka 2022. Bayern wamemng’oa Anfield kwa Pauni milioni 65.5.
Maisha yake ndani ya Anfield yalianza vizuri, kabla ya kiungo wa pembeni huyo kuharibiwa na majeraha ya goti aliyopata msimu wa 2022-23 na kumfanya akose mechi 35.
JJON DURAN (VILLA – AL NASSR)
Mshambuliaji huyo aliondoka Aston Villa mwaka huu, akichoka kusugua benchi mbele ya Ollie Watkins chini ya kocha Unai Emery.
Al-Nassr ya Saudi Arabia, ambayo pia inaye Cristiano Ronaldo kikosini, ilimsajili mwaka huu kwa ada ya Pauni milioni 64.
Duran aliondoka Villa akiwa amefunga mabao 12 katika mechi 30. Ndiye aliyepachika bao pekee katika mchezo dhidi ya Bayern Munich.
JULIAN ALVAREZ (MAN CITY – ATLETICO)
Nyota huyo raia wa Argentina aliondoka Man City na kujiunga na Atletico Madrid kwa Pauni milioni 64 mwaka 2024.
Alvarez aliyesajiliwa na Man City akitokea River Plate ya Argentina, aliondoka Etihad na kutua La Liga akiwa amemaliza msimu na mabao 19 na ‘asisti’ 13.
ROMELU LUKAKU (UNITED – INTER)
Ni mwaka 2019, ambapo Inter walitumia Pauni milioni 63.3 kumng’oa straika huyo pale Old Trafford. Aliondoka Man United akiwa ameitumikia kwa misimu miwili tu.
Miaka miwili akiwa Inter chini ya kocha Antonio Conte, alisajiiwa na Chelsea kwa Pauni milioni 97.5.
Published:


