20.1 C
New York

Dk. Jafo ataka TBS kutoa elimu madhara ya unywaji pombe kupita kiasi

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kushirikiana na taasisi nyingine kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi, akisema hali hiyo inapunguza nguvu kazi ya Taifa.

Dk. Jafo ametoa agizo hilo leo Mei 15, 2025, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.

“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imebaini kwamba bado kuna changamoto kubwa ya unywaji wa pombe uliopitiliza katika jamii, hali ambayo inasababisha kupotea kwa nguvu kazi ya taifa,” amesema Dk. Jafo.

Alisema ni muhimu kwa taasisi zilizo chini ya wizara yake, hususan TBS, kuanza kampeni za kitaifa za utoaji wa elimu kwa umma juu ya madhara ya matumizi mabaya ya vileo.

“Sasa nazielekeza taasisi zangu kutoa elimu kwa umma kuhusu unywaji wa pombe. Niwaombe Watanzania tubadilishe tabia; unywaji wa kupindukia ni hatari sana kwa afya na ustawi wa taifa letu,” ameongeza.

Waziri huyo alisisitiza kuwa ulevi wa kupindukia si tu changamoto ya kiafya, bali pia ni kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wa nchi, kwani huathiri uzalishaji na ustawi wa familia nyingi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img