Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeeleza dhamira yake ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, kupitia mikakati madhubuti ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU nchini.
Akizungumza Juzi jijini Dodoma, katika kikao cha watumishi wa TACAIDS, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Catherine Joachim, amesema utafiti wa mwenendo wa UKIMWIwa 2022/23 umeonyesha kupungua kwa maambukizi ya VVU kutoka watu 72,000 kwa mwaka (2016/17) hadi 60,000 kwa mwaka. Hata hivyo, vijana hasa wa kike wameendelea kuwa kundi lililo hatarini zaidi.

Ili kuhakikisha maambukizi yanapungua zaidi, TACAIDS imeanzisha Kampeni ya “Tusonge na Samia Kutokomeza UKIMWI”, ambayo inalenga kutoa elimu kwa jamii, hasa kwa vijana na makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi.
“Kampeni hii itahamasisha uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI na kuongeza kasi ya kufanikisha malengo ya kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030,” amesema Dk. Joachim.
Aidha, TACAIDS imepanga kufanya uraghibishi kwa viongozi wa Mikoa na Serikali za Mitaa juu ya matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya VVU/UKIMWI (2022/23), ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Kwa mujibu wa TACAIDS, jitihada hizi zinahakikisha kuwa jamii inapata elimu sahihi na huduma bora za afya, huku ikihamasisha upimaji wa VVU, matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi (ARVs) na mbinu salama za kujikinga na maambukizi mapya.


