16.6 C
New York

Dili za usajili zilizoitia hasara Man City

Published:

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER City ilimwaga sokoni kiasi cha Pauni bilioni 1.2 kusajili kuanzia mwaka 2009 hadi 2018 na uwekezaji huo haukwenda bure. Klabu hiyo ilitwa mataji makubwa saba ndani ya kipindi hicho.

Licha ya kwamba ilipata mafanikio hayo, haimaanishi kuwa hakuna wachezaji waliosajiliwa kwa fedha nyingi na wakashindwa kuwika.

Ni kama ilivyotokea kwa Omar Marmoush, Kalvin Phillips, Nico Gonzalez na Savio kwa miaka michache ya hivi karibuni.

ELIAQUIM MANGALA

Mwaka 2014, Man City walitumia Pauni milioni 42 na Mangala akawa mmoja ya mabeki wa bei mbaya katika historia ya Ligi Kuu ya England (EPL).

Alisajiliwa akitokea Porto ya Ureno lakini baada ya kucheza vizuri katika mechi yake ya kwanza (dhidi ya Chelsea), Mfaransa huyo akapoteana.

Akiishia kutolewa kwa mkopo katika klabu za Valencia na Everton, kabla ya Man City kumuuza mwaka 2019 kwa klabu hiyo ya Hispania.

STEVAN JOVETIC

Alisajiliwa mwaka huo huo, 2014, akitokea Fiorentina ya Italia kwa ada ya Pauni milioni 22. Ni kipindi ambacho Man City iliwasajili pia Fernandinho, Jesus Navas, Martin Demichelis na Alvaro Negredo.

Kwa Jovetic, ulionekana ni usajili wa kuziba mapengo ya washambuliaji wawili, Carlos Tevez na Mario Balotelli, waliokuwa wameondoka Etihad.

Misimu yake miwili klabuni hapo haikuwa mizuri kutokana na wimbi la majeraha na hatimaye akauzwa Inter Milan mwaka 2015 akiwa ameifungia Man City mabao 11 pekee katika mechi 44.

WILFRIED BONY

Man City walikubali kuipa Swansea City kiasi cha Pauni milioni 25 baada ya mshambuliaji huyo kufunga mabao 20 ya Ligi Kuu ya England. Hiyo ilikuwa mwaka 2015.

Achana na wimbi la majeraha, ushindani wa namba mbele ya straika raia wa Argentina, Sergio Aguero, viliyafanya maisha ya Bony yawe magumu Etihad.

Hatimaye, Bony aliondoka Man City akiwa amefunga mabao 10 pekee katika mechi 46 alizocheza katika michuano mbalimbali.

NOLITO

Ulionekana ni usajili bora pale Guardiola alipomchukua kutoka Celta Vigo mwaka 2016 baada ya winga huyo kufanya vizuri Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).

Mambo yakawa tofauti. Nolito alicheza Man City msimu mmoja tu, kisha akaondoka zake akiwa amecheza mechi tisa tu za Ligi ya England (EPL).

Aliporudi Hispania na kujiunga na Sevilla, alisema sababu ya kufeli EPL ni familia yake kutokuyapenda maisha ya England.

DANILO

Man City ilitumia kitita cha Pauni milioni 26.5 kumsajili akitokea Real Madrid na hiyo ilikuwa mwaka 2017 lakini alidumu klabuni hapo kwa misimu miwili pekee, akicheza mechi 34 za EPL.

Ni baada ya beki huyo kupoteza nafasi ya kuanza kikosini, ndipo Man City ilipomfanya ‘chambo’ katika dili la kumsajili Joao Cancelo kutoka Juventus mwaka 2019.

BENJAMIN MENDY

Akitokea Monaco, usajili wake uliigharimu Man City kiasi cha Pauni milioni 52, hivyo Mendy akawa beki ghali zaidi wakati huo.

Hata hivyo, beki wa kulia huyo aliishia kucheza mechi 75 tu akiwa Man City, kabla ya kuondoka klabuni hapo Juni, 2023.

Related articles

Recent articles