LONDON, Uingereza
ARSENAL haijafunga bao la kipindi cha kwanza katika mechi tano mfululizo ilizocheza hivi karibuni, iwe kwenye Ligi Kuu au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Washika Bunduki walipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Lille jana Oktoba 13, 2026, lakini yote yalipatikana kipindi cha pili, wafungaji wakiwa ni Jurrien Timber, Eberechi Eze na Bukayo Saka.
Kabla ya kukutana na Lille, Arsenal haikupata bao ndani ya dakika 45 za kwanza katika mechi zingine nne dhidi ya Napoli, Sunderland, Brighton na Leeds United.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa kocha Mikel Arteta anahitaji kuifanya kazi safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Kai Havertz na Viktor Gyokeres.
Pia, tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita [2025-26], Arsenal imepoteza uwezo wake wa kutegemea mipira iliyokufa. Haijafunga bao lolote kwa staili hiyo kwenye Ligi msimu huu.


