MIAMI, Marekani
AFRIKA haina mwakilishi katika hatua ya nusu fainali ya msimu huu wa Kombe la Dunia. Ni timu za Bara la Ulaya pekee zilizobaki.
Hata hivyo, ukiitazama safu ya ushambuliaji ya timu ya soka ya Taifa ya Ufaransa, kuna Kylian Mbappe, Ousmane Dembele, Michael Olise, na Eduardo Camavinga.
Kwa Mbappe, baba ni Mcameroon na mama ni raia wa Algeria. Dembele, baba ana asili ya Mali na mama ni Mauritania. Wazazi wa Olise wana asili ya Nigeria. Camavinga, wazazi wake wana asili ya DRC na Angola.
Katika kikosi cha England, kuna Bukayo Saka, ambaye wazazi wake wana asili ya Nigeria, Eberechi Eze (Nigeria) na Noni Madueke (Nigeria na DRC).
Wakati nyota hao wakizisaidia timu za Ulaya kutamba msimu huu wa Kombe la Dunia, mataifa yao ya asili (Cameroon, Mali, Nigeria, Angola na Mauritania) hayakufuzu kabisa.
Hata hivyo, licha ya kukubaliana kuwa Afrika ina vipaji vikubwa vya soka, wachambuzi wanaamini bado Ulaya kuna mazingira mazuri zaidi ya kuzalisha ubora wa wachezaji.
Kwamba wakati Afrika ikibaki kutegemea vipaji vya kuzaliwa, Ulaya imesogea zaidi na kujenga mifumo ya kutengeneza watu.
Mathalan, Ufaransa pekee Ina vituo vya kuibua na kuendeleza vipaji vya soka zaidi ya 3,000. Na hivyo ni vyenye leseni. Ni kama ilivyo Ujerumani, ambayo Chama cha Soka pekee kina vituo 366 vinavyofanya kazi na klabu za Ligi Kuu.
Sambamba na hilo, kila mchezaji chipukizi mwenye umri chini ya miaka 12 nchini Ufaransa ameingizwa kwenye mfumo wa tanzu-data (database) wa Shirikisho la Soka nchini humo (FFF).
Katika mazingira hayo, ni wazi leo hii Mbappe asingekuwa huyu wa leo endapo angebaki mjini Yaounde bila kupita katika ‘academy’ ya Taifa ya Ufaransa (Clairefontaine).
Saka hakufika hapa alipo akiwa Lagos, bali alipita katika academy ya Arsenal pale London, ambapo hata kinda wa umri chini ya miaka 9 ana utaratibu maalumu, ikiwamo aina ya vyakula anavyopaswa kutumia.
Olise wa leo hakufika hapo akiwa Abuja. Alitengenezwa na academy za Reading na Crystal Palace, akisimamiwa na wataalamu, wakiwamo wanasayansi wa michezo na mawakala wanaotambuliwa na FIFA.
Pia, kama zinavyofanya England na Ujerumani, Ufaransa nayo ina mfumo wa ‘Disapora Unit’, ambao kazi yake ni kufuatilia vizazi vyenye asili ya nchi yao katika mataifa mbalimbali duniani.
Kupitia mfumo huo, Ufaransa imekuwa ikiwapa uraia-pacha makinda wenye umri kuanzia miaka 15, pia ikituma maskauti wake kuwafuatilia katika mingi Afrika, ikiwamo Bamako, Dakar na Lagos.


