24.3 C
New York

Cape Verde wanasa kwa Argentina; watatoboa kweli?

Published:

MEXICO CITY, Mexico

BAADA ya kuvuka hatua ya makundi, sasa timu ya soka ya Taifa ya Cape Verde imeangukia kwa mabingwa watetezi wa msimu huu wa Kombe la Dunia, Argentina.

Baada ya suluhu (0-0) dhidi ya Saudi Arabia, Cape Verde walikuwa wakiiombea ushindi Hispania iliyokuwa ikicheza na Uruguay.

Hivyo, baada ya Hispania kushinda bao 1-0, Cape Verde imefanikiwa kutinga hatua ya 32 Bora ikiwa nafasi ya pili kwenye Kundi H.

Ni kwa maana hiyo sasa, Cape Verde itakwaana na Argentina ya Lionel Messi katika mchezo wa Ijumaa ya wiki ijayo mjini Miami, Marekani.

Kocha wao, Bubista, amesema hawana cha kuhofia katika mchezo huo. “Kwa upande wetu, hakuna kinachoshindikana. Tangu mwanzo, tulishasema nia yetu ya kujitangaza nchi yetu duniani,” amesema.

Naye kiungo wa timu hiyo, Deroy Duarte, ambaye alitwaa tuzo ya nyota wa mchezo dhidi ya Saudia, amesema:

“Kuanzia sasa, tunajipanga kwa mchezo ujao. Dhidi ya Argentina, siyo? Ni mechi ngumu lakini bado tuna imani. Hakuna kinachoshindikana.”

Mkongwe wa Manchester United na timu ya soka ya Taifa ya England, Gary Neville, ni miongoni mwa waliovutiwa na mafanikio ya Cape Verde.

“Nafikiri waliokuwa wanaponda timu kuongezwa (na kufikia 48) wanapaswa kujifikiria tena kwa kutazama timu kama Cape Verde.

“Nchi yenye watu 500,000 inafika hatua ya mtoano. Tumeshuhudia Uruguay, moja ya nchi kubwa, ikitolewa na timu ndogo ikisonga mbele. Ni upekee wa aina yake,” amesema.

Related articles

Recent articles