NEW YORK, Marekani
FAINALI za Kombe la Dunia zina siku chache tu tangu zianze Juni 11, 2026, zikifanyika katika mataifa matatu; Marekani, Canada na Mexico.
Licha ya kwamba ni mechi chache zilizochezwa, tayari zimeshuhudiwa rekodi kadhaa zikivunjwa.
CANADA NA POINTI MOJA
Katika historia ya Kombe la Dunia, safari hii timu ya soka ya Canada imefanikiwa kwa mara ya kwanza kupata walau sare (pointi moja).
Pointi moja hiyo ilipatikana katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Bosnia. Canada ilifungwa mechi zote tatu wakati wa fainali za mwaka 1986, kama ilivyokuwa mwaka 2022.
QATAR WAMEJIPATA
Waliposhiriki kwa mara ya kwanza wakiwa wenyeji mwaka 2022, walichezea vichapo katika mechi zote tatu za hatua ya makundi. Safari yao ikaishia hapo.
Msimu huu, timu ya soka ya Taifa ya Qatar imekuja tofauti na kupata sare yao ya kwanza ya Kombe la Dunia. Sare ya bao 1-1 dhidi ya Uswis katika mechi yao ya kwanza.
‘MVUA’ YA KADI NYEKUNDU
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, msimu huu umeshuhudia kadi nyekundu tatu kwenye mechi ya ufunguzi.
Hilo lilitokea wakati Mexico walipovaana na wakongwe soka la Afrika, Afrika Kusini. Wenyeji walipata moja, huku mbili zikielekea kwa ‘Wasauzi’.
MIAKA 36 YA SCOTLAND
Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990, timu ya Taifa ya Scotland ilipata ushindi wake wa mechi za Kombe la Dunia. Ni baada ya kuifunga Haiti bao 1-0.
Kabla ya mchezo huo, Scotland hawakuwa wameshinda hata mechi moja katika misimu minne ya Kombe la Dunia, sawa na miaka 36 tangu walipoifunga Sweden (Juni 16, 1990).
MOROCCO YAENDELEZA NUKSI
Sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil ni mwendelezo wa timu ya soka ya Morocco kukosa ushindi katika mechi zake za kwanza Kombe la Dunia.
Kabla ya kukutana na mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia (Brazil), Morocco ilifungwa mara tatu na kutoa sare tatu katika michezo yao ya ufunguzi.


