TORONTO, Canada
KATIKA mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kati ya timu ya soka ya Taifa ya Brazil na Morocco, kinda Ayyoub Bouaddi alikuwa sehemu ya safu ya kiungo ya kikosi cha vigogo hao wa soka la Afrika.
Ikiwa ni mechi yake ya kwanza akiwa na ‘uzi’ wa Morocco, Bouaddi (18), alimpa wakati mgumu Casemiro, ambaye akimaliza dakika 45 za kwanza akiwa amegusa mpira mara 18 pekee.
Akionekana kuzidiwa, mkongwe huyo aliitwa benchi na kumpisha Fabinho, ambaye pia hakuweza kutamba mbele ya ‘dogo’ huyo.
Bouaddi anayekipiga Lille ya Ligue 1, alishacheza U-21 ya Ufaransa lakini aliamua kugeuka na kuiwakilisha Morocco, ambapo alitumika katika mechi tatu za kujiandaa na Kombe la Dunia.
Katika mechi 96 alizocheza katika misimu mitatu ya hivi karibuni akiwa na kikosi cha Lille, 63 ni za Ligi Kuu (Ligue 1).
Arsenal wamekuwa wakimfuatilia kwa miezi mingi ya hivi karibuni, ikiripotiwa kuwa klabu hiyo imezungumza mara kadhaa na wawakilishi wake.
Liverpool chini ya kocha mpya, Andoni Iraola, nayo inamtolea macho, kama ilivyo kwa Man United iliyompa mkataba mpya wa miaka miwili Michael Carrick.
Wakati huo pia, PSG nao wameripotiwa kuitaka saini ya Bouaddi, huku Lille wakitajwa kuhitaji si chini ya Pauni milioni 60 ili kumwachia nyota wake huyo.


