17.4 C
New York

Kombe la Dunia 2026: Karata ya mwisho kwa Cristiano Ronaldo

Published:

LISBON, Ureno

KAMA kuna mchezaji anayezitamani zaidi fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu, 2026, basi ni nahodha wa timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo.

Mosi, licha ya kwamba ameshiriki mara tano, staa huyo wa Al Nassr ya Saudi Arabia hajawahi kutwaa taji hilo, licha ya heshima kubwa, vikombe vingi na tuzo nyingi alizowahi kupata katika ngazi ya klabu.

Pili, mpinzani wake mkubwa katika ulimwengu wa mchezo wa kandanda, Lionel Messi, alitwaa taji hilo msimu uliopita, 2022, nchini Qatar.

Baada ya kila mmoja kuwa na mafanikio makubwa, Ronaldo anaonekana kukosa nguvu mbele ya Messi linapokuja suala la kutwaaa ubingwa wa Kombe la Dunia.

Tatu, Ronaldo atashiriki fainali za mwaka huu akiwa na kumbukumbu mbaya ya kufunga bao moja pekee msimu uliopita wa Kombe la Dunia.

Kama hiyo haitoshi, hakufunga hata bao moja licha ya kuanza katika mechi zote tano za fainali za EURO zilizopita za mwaka 2024.

Nne, ni wazi hizi ni fainali zake za mwisho. Atashiriki akiwa na umri wa miaka 41. Kwa ufupi, hii inaweza kuwa hatua yake ya mwisho akiwa na timu ya Taifa.

Tano, licha ya Ureno kushiriki mara nane Kombe la Dunia, mafanikio pekee wanayojivunia ni kushika nafasi ya tatu na hiyo ilikuwa mwaka 1966.

Ureno ambayo inakwenda kwenye mashindano ikiwa na safu bora ya kiungo yenye Bruno Fernandes, Vitinha, Joao Neves na Bernardo Silva itafanya maajabu gani safari hii?

Watatupa karata yao ya kwanza Juni 17, 2026 kwa kuivaa DRC, kabla ya kuzivaa Uzbekistan na Colombia katika michezo mingine ya Kundi K.

Related articles

Recent articles