22.9 C
New York

Visualization| Serikali inavyovuna fedha kwenye michezo ya kubahatisha

Published:

UKWELI usio na shaka ni kwamba sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini imeonekana kupiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo, ukuaji huo kama ilivyoonekana mwaka 2018/19 haukuwa wa bahati mbaya, bali ulitokana na mikakati ya Serikali na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kile kinachoakisi jitihada za Serikali, sekta hiyo imeandaliwa mazingira rafiki, kubwa ikiwa ni kuhakikishiwa ulinzi wa kisheria.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe, ukuaji wa sekta hiyo unaweza kuonekana wazi kupitia mambo mawili;

Mosi, ni kutanuka kwa biashara za wale waliokuwa na leseni. Kwamba kama alikuwa na kituo kimoja, sasa ameanzisha kingine kutokana na utitiri wa wateja.

Pili, ni ongezeko la watoa huduma wapya waliotapakaa nchi nzima.

“Hii inatokana na uwapo wa mazingira rafiki, ikiwamo mfumo mzuri wa sheria zinazosimamia. Kwa mwaka 2018/19, kulikuwa na ongezeko la asilimia 20.69% katika ukusanyaji wa kodi inayotokana na michezo ya kubahatisha.

“Hilo ni ongezeko kutoka bilioni 78.8 zilizoingia mwaka 2017-18 hadi bilioni 95.1 za mwaka 2018-19,” amesema Mbalwe.

Aidha, Mbalwe amesema ongezeko la wawekezaji kwenye sekta hii limechagiza ukuaji wa uchumi wa nchini.

Katika hilo, amesema kodi zitokanazo na sekta ya michezo ya kubahatisha imepanda kwa asilimia 520.15 ndani ya miaka mitano, yaani kutoka bilioni 15.33 mwaka 2014/15 hadi bilioni 95.07 mwaka 2018/19.

“Ukusanyaji wa kodi za michezo ya kuhabatisha umekuwa ukipanda kila uchwao. Kwa mwaka 2018/19, Serikali ilikusanya bilioni 95.1, hilo ni ongezeko la asilimia 21.51 ukilinganisha na bilioni 78.76 zilizokusanywa mwaka 2017-18,” amesisitiza.

Vilevile, mbali ya kusema sekta hii imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa kigeni, pia Mbalwe akagusia namna ilivyochagiza ongezeko la ajira nchini.

“Sekta ya michezo ya kuhabatisha inaendelea kuzalisha ajira kwa watu wetu. Watanzania wengi wameajiriwa katika kampuni nyingi tu za kubashiri. Wapo wanaolipwa kwa mwezi, wengine wanapata posho tu,” amesema na kuongeza:

“Jumla ya watu walioajiriwa kwenye sekta hii ya michezo ya kubahatisha inakadiriwa kufikia 20,000 kwa mwaka 2018-19…”

Licha ya faida lukuki hizo, zipo sheria zinazoongoza michezo ya kubashiri nchini, lengo likiwa ni kudhibiti vitendo vinavyoweza kuwa hatarishi kwa jamii (washiriki).

Mathalan, Serikali inapinga vikali ushiriki wa mtoto (mtu mwenye umri chini ya miaka 18) kwenye aina yoyote ya michezo ya kubahatisha.

“Ni muhimu kusisitiza kwamba watu walio chini ya umri wa miaka 18 hawaruhusiwi kushiriki kwenye michezo ya kubashiri. Kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Michezo ya Kubashiri ya mwaka 2003, watoto wanazuiwa kuingia kwenye shughuli za ubashiri…” anasema Mbalwe.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img