Mwandishi Wetu, Gazetini – SHINYANGA
KATIKA kikao kazi cha kutathmini maendeleo ya upatikanaji wa maji maeneo ya mjini na vijijini mkoani Shinyanga, Diwani kata ya Solwa Dotto Samson ameshauri Mamlaka za maji kuweka mfumo wa malipo ya maji kama mita za ‘Luku’ ili kutatua tatizo la watu wenye madeni kupelekea wengine wasio na madeni kukosa maji.
Hayo yamesema leo, Jumatatu, Novemba 16, 2026 katika kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga iliyopo Manispaa ya Shinyanga, huku akihoji kutofautiana kwa gharama za malipo ya maji kwa Vyombo vya utoaji huduma ya maji kwa jamii (CBWSOs) kati ya kata na kata ikiwa huduma ni ileile katika kata hizo na ni Halmashauri moja,
“Niliwasiliana na Diwani wa kata ya Mwantini akaniambia wanalipa 2,500 wakati wengine tunalipa 1,500 hadi 1,700, inakuwaje kunakuwa na utofauti wa gharama wakati huduma ni ileile na ni ndani ya Halmashauri moja? Naomba bei iwe moja” amesema Samson.

Naye Mbunge wa jimbo la Itwangi Azza Hillal ameshauri kuwa ripoti za upatikanaji wa maji zipangwe kijimbo na sio Halmashauri kwa sababu halmashauri zingine zina jimbo zaidi ya moja na jimbo lingine maji yanapatikana na pengine maji hayapatikani kabisa,
“Mnaposema Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga upatikanaji wa maji ni asilimia 79.3, mimi nakataa kwa sababu Itwangi kuna shida ya maji kuliko jimbo lolote niwaombe hizi ripoti ziwe zinaandaliwa kwa jimbo na sio halmashauri, pia kuna mradi wa maji kata ya Bukene umekamilika lakini wananchi hawapati huduma ya maji” amesema Azza.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Emaeli Nkopi ameeleza kuwa, “Tofauti ya gharama ya malipo inategemeana na CBWSO yenyewe inayohudumia eneo husika lakini tofauti huwa sio kubwa, lakini hii ya 1500 hadi 2500 inashangaza hili suala lakini hii inatokana na mtiririko kwa kuuza maji kutoka Kashuwasa kwenda Shuwasa hadi kufika kwenye CBWSOs zetu lakini hili tatizo linakwenda kuisha tutauziwa maji moja kwa moja kutoka Shuwasa”
Pia ameongeza kuwa, “Suala la kutofautisha ripoti kijimbo tumelichukua na nihaidi kikao kijachao ripoti zetu zitaandaliwa liwa kijimbo na sio halmashauri tena, pia mradi wa maji kata ya Bukene kweli umekamilika lakini tuko kwenye majaribio ya mwisho na hivi karibuni utakabidhiwa na wananchi wataanza kupata huduma ya maji nikutoe wasiwasi” amesema Nkopi.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amewataka mamlaka za maji kuhakikisha maeneo ya vijijini hasa yale ya mbali yanafikiwa maji kwa kasi ileile, na yenye kukidhi mahitaji ya wananchi wote.


