PARIS, Ufaransa
POLISI nchini Ufaransa wamelazimika kuingilia kati maandamano makubwa yanayoongozwa na wanafunzi wanaolalamikia ubora wa elimu. Maandamano hayo yamesababisha shule zaidi ya 700 kutokuendelea na masomo.
Waandamanaji hao, wengi wakiwa ni wanafunzi wa sekondari, wamelalamikia uhaba wa waalimu katika shule nyingi na idadi kubwa ya wanafunzi darasani.
Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurent Nunez, ameeleza kuwa tayari polisi wanawashikilia watu 1,747 waliokuwamo kwenye maandamano hayo.
Maandamano yalianza wiki iliyopita mjini Paris na sasa yameenea katika miji mbalimbali, ikiwamo ya Montpellier, Nantes na Marseille.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria, Gerald Darmanin, amesema maandamano hayo yalianzishwa na wanafunzi lakini sasa yamevuna ushawishi wa makundi mengine kwenye jamii.


