CALIFORNIA, Marekani
UNAMFAHAMU Andrew Cherng? Ndiye mmiki wa kampuni maarufu ya Panda Express, ambayo ina migahawa yake mingi katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa sasa, Cherng ana umri wa miaka 78 na yeye na mkewe, Peggy, wana utajiri wa Dola za Marekani bilioni 6.6.
Tofauti na wengine waliozaliwa kwenye familia tajiri, Cherng ametengeneza pesa zake pasi na kutegemea baba na mama. Kwa ufupi, ametengeneza utajiri Katikati ya umasikini.
Iko hivi; alizaliwa mwaka 1948 mjini Yangzhou, China. Akiwa na umri wa miaka mitano, familia yake ilihamia Taiwan, na miaka nane baadaye walihamishia makazi nchini Japan.
Miaka mingi baadaye, alihamia Marekani kwa ajili ya masomo katika Chuo Kikuu cha Baker mjini Kansas, ambako alisomea Hisabati. Akiwa huko, alikutana na Peggy, ambaye ndiye mkewe kwa sasa na ‘CEO’ mwenzake katika Kampuni ya Panda Express.
Hata hivyo, ilihitaji vita ya jasho na damu kufikia utajiri alionao leo. “Kila kilipofika kipindi cha likizo, nilikuwa nafanya kazi New York. Nilikuwa nahudumia katika migahawa. Baba yangu alikuwa mpishi lakini hakuwahi kumiliki biashara yake.
“Sikuipenda hali hilo. Moyoni mwangu, nilijua nataka kuwa kwenye biashara,” alisimulia Cherng mwaka 2013 alipofanyiwa mahojiano maalumu na jarida kongwe la Forbes.
Walipomaliza Shahada ya Uzalimili (Master’s Degree), Peggy aliendelea na Shahada ya Uzamivu, lakini Cherng Aliona ni wakati sahihi wa kuianza safari yake kwenye biashara.
Alianza kwa kuajiriwa na binamu yake katika mgahawa mjini California, wakati huo Cherng akilipwa mshahara kiduchu wa Dola za Marekani 800 tu kwa mwezi.
Mwaka uliofuata, alikaa chini na wazazi wake wakiwa na kiasi cha fedha kinachofikia Dola 60,000 walichokipata kwa kudundulika na mkopo kidogo kutoka katika moja ya taasisi za fedha.
Wakafungua Mgahawa wa Panda mwaka 1973. Akisimulia hali ya kiuchumi ilivyokuwa mbaya, Cherng alisema: “Familia nzima, kuanzia wazazi, kaka na dada yangu, tulifanya kazi bila malipo katika mgahawa huo.
“Tulikuwa tunaishi kwenye nyumba yenye vyumba viwili, hatukuwa na pesa. Peggy alikuwa anakuja kututembelea, kisha tukafunga ndoa mwaka 1975.”
Cherng anasema kufikia mwaka 1983, kwa mara ya kwanza, waliweza kufungua mgahawa wa Panda Express ndani ya moja ya majengo makubwa ya biashara ya California. “Mwaka 1985, Panda iliongeza matawi kutoka matano hadi tisa,” alisema.
Leo hii, Panda Express ina matawi zaidi ya 2,600 duniani kote, ikiwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 55,000. “Kwa mwaka 2025 pekee, tulihudumia kuku zaidi ya milioni 148,” alisema Cherng.


