YOUNDE, Cameroon
TIMU ya soka ya Taifa ya Cameroon haikufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) lakini lejendari wake, Rigobert Song, ana rekodi yake inayoendelea kuishi kwenye historia ya michuano hiyo.
Song aliyezaliwa Julai Mosi, 1976, mjini Younde, aliwahi kutamba Ulaya akiwa na klabu za Liverpool, West Ham United, Koln, Lens, Galatasaray, na Trabzonspor.
Kwa upande mwingine, ndiye mchezaji mwenye mechi nyingi (137) katika historia ya timu ya soka ya Taifa ya Cameroon.
Pia, kwa Kombe la Dunia, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kupewa kadi nyekundu katika historia ya mashindano hayo. Hiyo ilikuwa mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka 17.
Wakati huo huo, ukiacha Zinedine Zidane ‘Zizou’, Song ndiye mchezaji pekee aliyewahi kupewa ‘umeme’ (kadi nyekundu) katika misimu miwili tofauti ya Kombe la Dunia.
Akipewa kadi yake ya kwanza katika mchezo dhidi ya Brazil (1994), kisha nyingine ikafuata walipokutana na Chile (1998).
Kwa ujumla, Song alistaafu akiwa amecheza misimu minne ya Kombe la Dunia (1994, 1998, 2002 na 2010).
Kwa sasa, lejendari huyo aliyepachikwa jina la ‘Big Chief’ alipokuwa Trabzonspor ya Uturuki, ni kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ifahamike kuwa Song ni mjomba wa ‘mido’ wa zamani wa Arsenal na timu ya soka ya Taifa ya Cameroon, Robert Song.


