20.7 C
New York

Kibarua wa viwandani aliyefunga mabao mawili kuiokoa Ujerumani

Published:

MEXICO CITY, Mexico

IVORY Coast ikiwa mbele kwa bao 1-0, kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Ujerumani, alimuinua kwenye benchi Deniz Undav aliyeingia na kufunga mabao mawili katika mchezo huo wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea.

Mechi ikamalizika kwa Ujerumani kushinda mabao 2-1 na kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014.

Katika mechi mbili, ambazo zote ametokea benchi msimu huu wa Kombe la Dunia, amehusika katika mabao matano, akifunga matatu na kutoa asisti mbili.

Kwa mabao yake dhidi ya Ivory Coast, nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa mchezaji wa kwanza wa Ujerumani kufunga katika michezo miwili ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu Miroslav Klose alipofanya hivyo mwaka 2002.

Nje ya mabao, asisti na rekodi yake hiyo, Undav ana historia yake ya kuumiza. Akiwa na umri wa miaka 14, alikataliwa na ‘academy’ ya Werder Bremen.

Akiwa na miaka 17, akawa na timu ya ‘mchangani’ (Daraja la Nne) nchini Ujerumani, huku alifanya kazi kiwandani ili kupata fedha za kujikimu.

“Nikiwa na miaka 14, Werder walinikataa wakisema nina umbo dogo. Iliniumiza,” anasimulia nyota huyo.

“Sikukata tamaa. Niliondoka nyumbani na kwenda kusajiliwa na timu ya Daraja la Nne, ambapo nilifanya mazoezi, huku nikienda kiwandani nilikokuwa naendesha mashine.”

Anasema alikuwa akiamka saa 10 alfajiri na kwenda kiwandani, kisha kuunganisha mazoezini saa 8 mchana, kabla ya kurudi nyumbani saa 2 usiku.

“Nililazimika kufanya kazi (kiwandani) ili kupata fedha za kuendesha maisha. Katika soka sikuwa nalipwa fedha za kutosheleza mahitaji,” anasema.

Mwaka 2020, Undav alisajiliwa na Union Saint-Gilloise ya Daraja la Pili nchini Ubelgiji, kabla ya kutua Brighton ya England msimu wa 2022-23.

Aliumaliza msimu huo akiwa na mabao matano katika mechi 22 za Ligi Kuu ya England (EPL), hivyo akatolewa mkopo Stuttgart iliyomsajili moja kwa moja mwaka 2024.

Msimu uliomalizika, 2025-26, alifunga mabao 19 ya Bundesliga, akiwa nafasi ya pili nyuma ya Harry Kane aliyetwaa kiatu cha ufungaji bora.

Related articles

Recent articles