BAGHDAD, Iraq
MOJA ya vivutio vya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zitakazoanza Juni 11, 2026 ni uwepo wa timu ya soka ya Taifa ya Iraq iliyofuzu kwa kuifunga Bolivia. Hii inakuwa mara ya pili kwao kushiriki baada ya mwaka 1986.
Katika mashindano hayo, Iraq iliishia hatua ya makundi kwa kupoteza mechi zote tatu dhidi ya Paraguay, Ubelgiji na wenyeji Mexico.
Safari hii, bado Iraq wana kazi kubwa ya kufanya kwani wamepangwa tena katika kundi gumu lenye Ufaransa, Senegal na Norway.
Timu ya Taifa hilo la Kiarabu lenye watu milioni 46 itatupa karata yake ya kwanza Juni 16, 2026 kwa kuivaa Norway inayoongozwa na straika tishio Ligi Kuu ya England, Erling Haaland.
NDOTO ILIYOTIMIA KATIKATI YA VITA
Kwa miaka mingi, Iraq imekuwa ikitawaliwa na hali mbaya ya usalama, ikitajwa kuwa sababu ya nchi hiyo kuchelewa kurudi Kombe la Dunia tangu iliposhiriki mwaka 1986.
Machafuko yasiyokoma yaliathiri mara kadhaa maandalizi ya timu ya taifa kuelekea mechi zake za kufuzu. Kutokana na vita, ni kwa miaka mingi sasa timu ya haijacheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia katika ardhi ya Mji Mkuu, Baghdad.
Na badala yake, timu ya Taifa ya Iraq ilitumia nchi jirani za Jordan, Iran na Malaysia kwa mechi za nyumbani, hadi pale FIFA ilipoiruhusu kutumia Mji wake wa Basra mwaka 2020.
Kuelekea mechi yao ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu dhidi ya Bolivia, machafuko ya Mashariki ya Kati yalikaribia kuifanya timu yao ishindwe kusafiri kwenda Mexico.
Kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran, wachezaji na kocha wa Iraq, Arnold, walipata wakati mgumu kuondoka nchini humo kwenda Mexico ilikochezwa mechi hiyo.
KIKOSI CHA MASTAA, MATARAJIO
Tofauti na ilivyokuwa mwaka 1986, kwa sasa timu ya Taifa ya Iraq imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa wachezaji wake wanaocheza soka barani Ulaya.
Baadhi yao ni Ali Al-Hamadi wa Ipswich Town, Zidane Iqbal aliyewahi kupita Manchester United na sasa Utrecht ya Uholanzi, na Kevin Yakob aliyetoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Denmark akiwa na klabu ya AGF.
Katika benchi la ufundi, kocha ni Graham Arnold, ambaye mwaka 2022 aliiongoza Australia kuingia hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia.
Mwandishi wa habari za michezo maarufu wa Iraq, Nawar Faeq Al-Rikabi, amesema: “Watu wanatuona kama timu dhaifu zaidi kwenye kundi lakini mambo yanaweza kuwa tofauti.
Akizungumzia uwepo wa kocha Arnold, Al-Rikabi amesema wana matumaini makubwa, wakikumbuka Argentina ilivyopata usindi wa mbinde mbele ya Australia yake mwaka 2022. “Ni mzoefu na naamini tutafanya vizuri sana,” amesema.


