20.9 C
New York

Carlo Ancelotti na ‘mzimu’ wa Neymar, kikosi cha mastaa Brazil

Published:

RIO, Brazil

UNAPOITAJA timu ya soka ya Taifa ya Brazil, unazungumzia mabingwa mara nyingi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia. Wamelibeba taji hilo mara tano.

Hata hivyo, tofauti na miaka mingi iliyopita, kwa sasa ni kama heshima yao kwenye michuano hiyo imeporomoka. ‘Selecao’ (Wateule) wamepoteza ufalme wao.

Safari hii, kocha ni mkongwe Carlo Ancelotti, mmoja ya makocha wenye hadhi na heshima kubwa katika ulimwengu wa kandanda, akiwahi kuzinoa kwa mafanikio makubwa klabu nyingi, zikiwamo AC Milan na Real Madrid.

Ancelotti ameshaita kikosi chake cha wachezaji 26 atakaokwenda nao Kombe la Dunia mwaka huu, fainali hizo zikitarajiwa kuanza Juni 11, 2026.

Gumzo ni uwepo wa jina la Neymar, ambaye wakosoaji wake wanaona hawezi kuisaidia timu kutokana na kiwango chake kushushwa na majeraha ya mara kwa mara kwa miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo, Ancelotti, ambaye awali alisema hawezi kumwita kikosini mchezaji asiye na utimamu, amemtetea staa huyo mwenye umri wa miaka 34, akisema atakuwa na mchango mkubwa huko Marekani, Canada na Mexico.

Kwa upande mwingine, Muitalia huyo ameita kikosi kinachowapa matumaini makubwa mashabiki wa Brazil, amabacho kimejaa wachezaji wanaofanya vizuri barani Ulaya.

Baadhi yao ni makipa wawili tishio, Alisson na Ederson, mabeki Gabriel Magalhaes na Marquinhos, viungo Bruno Guimaraes, Casemiro, Fabinho, Lucas Paqueta, na washambuliaji Gabriel Martinelli, Matheus Cunha, Raphinha, na Vinicius Jr.

HIKI HAPA KIKOSI CHA KWANZA

Ni wazi Ancelotti atachagua kuanza na kipa wa Liverpool, Alisson Becker, akisaidiwa na mabeki  Santos, Gabriel, Marquinhos na Wesley.

Katika eneo la kiungo, uwezekano ni mkubwa kwa kocha huyo kumpa nafasi mkongwe Casemiro, akicheza na Guimaraes katika pacha ya kiungo.

Ni katika kikosi hicho, Martinelli na Raphinha watatumika kama winga, huku Vinicius Jr na Cunha wakicheza ndani, kwa maana ya straika (namba 9)  na kiungo mshambuliaji (namba 10).

AWACHIMBIA MKWARA ‘MAFAZA’

Kocha huyo amesema lengo lake si kutwaa ubingwa, bali kuiona timu yake ikiwa na msimu mzuri kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia.

“Akili yangu haipo kwenye ubingwa. Ninachotaka ni kuona tunafanya vizuri,” amesema Ancelotti ambaye vijana wake watarusha karata yao ya kwanza Juni 13 kwa kuivaa Morocco.

Pia, kocha huyo anayefahamika kwa ukali wake, hasa kwa wachezaji wasio na nidhamu, amesema katika kikosi alichoita hakuna supastaa.

” … Hatuhitaji supataa. Hatuhitaji kuwa na mchezaji mkubwa kuliko wengine. Hatuwezi kuelekeza akili zote kwa mchezaji mmoja. Tunapaswa kuwa timu. Hiyo ndiyo njia pekee ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia,” alisema.

Related articles

Recent articles