MUNICH, Ujerumani
MABINGWA mara nne wa fainali za Kombe la Dunia, timu ya soka ya Taifa ya Ujerumani imekuwa na mkosi wa kuondoshwa mapema kwenye michuano hiyo kwa miaka ya hivi karibuni.
Katika fainali za mwaka huu zitakazoanza Juni 11, Ujerumani imepangwa Kundi E ikiwa na Curacao, Ivory Coast and Ecuador.
Kwa misimu miwili mfululizo, 2018 na 2022, Ujerumani haijavuka hatua ya makundi. Kwa ufupi, tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2014.
Kuelekea michuano hiyo, hofu ni kubwa kwa mashabiki kwani timu yao ilipata ushindi kiduchu wa mabao 4-3 dhidi ya Uswis katika mchezo uliopita wa kirafiki uliochezwa Machi, 2026.
Kama hiyo haitoshi, Ujerumani inakwenda Kombe la Dunia ikiwa haijakutana na timu kubwa yoyote tangu mwaka jana ilipofungwa na Ufaransa na Ureno.
Ujerumani watafungua pazia la msimu huu wa Kombe la Dunia kwa kuivaa Curacao, ambayo hii ni mara yao ya kwanza kucheza mashindano hayo.
Ikiwa na watu 156,000, Curacao ndiyo nchi ndogo zaidi kuwahi kukata tiketi ya kucheza michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Licha ya ugeni wake, timu hiyo iko chini ya kocha mzoefu katika soka la Ulaya, Dick Advocaat, ambaye amerejea baada ya kujiuzulu Februari, 2026, kutokana afya ya binti yake kutetereka.


