12.9 C
New York

‘Majembe’ yaliyopigwa chini England itakayokwenda Kombe la Dunia 2026

Published:

LONDON, Uingereza

KOCHA wa timu ya soka ya Taifa ya England ‘Three Lions’, Thomas Tuchel, ameshatangaza kikosi chake kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zitakazoanza Juni 11 katika mataifa ya Marekani, Mexico na Canada.

England inakwenda kwenye michuano hiyo ikiwa na kiu ya kutimiza ndoto ya kulibeba taji hilo kwa mara ya kwanza tangu ilipofanikiwa mwaka 1966.

Hata hivyo, katika kikosi alichoita Tuchel raia wa Ujerumani, baadhi ya mastaa hawajapata nafasi, hivyo watazifuatilia fainali hizo wakiwa nyumbani.

NICK POPE (NEWCASTLE UNITED)

Tuchel amefanya uamuzi mgumu wa kutomjumuhisha kikosini mlinda mlango huyo, na badala yake amewaita Jordan Pickford, Dean Henderson na James Trafford.

Uamuzi huo umewashangaza wengi kwa kuwa Pope mwenye umri wa miaka 34 ndiye chaguo la kwanza katika kikosi cha Newcastle, akimpiga bao Aaron Ramsdale.

TRENT ALEXANDER-ARNOLD (REAL MADRID)

Majeraha ya mara kwa mara yamemponza beki huyo wa kulia wa Real Madrid. Amecheza mechi 14 pekee za La Liga msimu huu wa 2025-26.

Tuchel ameamua kwenda na Reece James na Tino Livramento, akimwacha Trent aendelee kujitafuta katika majeraha yake.

HARRY MAGUIRE (MAN UNITED)

Nyota huyo wa Manchester United alikuwa mchezaji muhimu kwenye eneo la beki wa kati wakati England ilipofika fainali ya Euro mara mbili mfululizo.

Maguire ameeleza kushitushwa na uamuazi wa kuchwa na Tuchel, hasa baada ya kiwango bora alichokionesha msimu huu chini ya kocha wa Man United, Michael Carrick.

ADAM WHARTON (C. PALACE)

Kiungo wa ulinzi ambaye amekuwa na kiwango bora msimu huu wa Ligi Kuu ya England akiwa na kikosi cha Crystal Palace.

Licha ya kiwango chake kuzivutia klabu kubwa, zikiwamo Manchester City, Liverpool na Chelsea, Tuchel ameamua kwenda na kiungo mkongwe, Jordan Henderson.

MORGAN GIBBS-WHITE (NOTTINGHAM FOREST)

Kwa kiwango chake msimu huu wa Ligi Kuu ya England na Ligi ya Europa, Gibbs-White alitarajiwa kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

Kiungo huyo amehusika katika mabao 18 ya Forest, akiiwezesha timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Europa, ambapo walifungwa na Aston Villa iliyokwenda kutwaa ubingwa.

COLE PALMER (CHELSEA)

Licha ya kiwango chake kizuri akiwa na Chelsea, mshambuliaji huyo ameshindwa kumshawishi Tuchel kumjuhuisha katika safari ya Kombe la Dunia.

Na badala yake, Tuchel, kocha wa zamani wa Chelsea, amechagua kwenda na Ivan Toney na Noni Madueke.

PHIL FODEN (MAN CITY)

Kwa miaka mingi ya hivi karibuni, winga wa kushoto huyo ameshindwa kuhamishia timu ya taifa makali anayokuwa nayo akiwa na kikosi cha Manchester City.

Mataji sita ya Ligi Kuu na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini bado si mchezaji tegemeo England, hivyo Tuchel ameamua kumuacha nyumbani.

DANNY WELBECK (BRIGHTON)

Akiwa na mabao 23 katika misimu miwili ya hivi karibuni Ligi Kuu ya England, straika huyo wa zamani wa Arsenal aliamini ana nafasi ya kwenda Kombe la Dunia.

Hata hivyo, Tuchel amechagua kwenda na Toney, ambaye ni mkali wa penalti na amefunga mabao 42 msimu huu wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

Related articles

Recent articles