Na mwandishi wetu, Gazetini
TANZANIA imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kivutio kikubwa cha uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya madini, baada ya kuorodheshwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza barani Afrika, kwa mujibu wa ripoti ya Fraser Institute, Annual Survey of Mining Companies 2025.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepanda hadi nafasi ya 34 kati ya maeneo 68 yaliyotathminiwa duniani katika Investment Attractiveness Index (IAI), kipimo kinachotumiwa na wawekezaji na kampuni za utafiti wa madini kuamua maeneo yenye mvuto mkubwa kwa uwekezaji wa utafiti na maendeleo ya miradi.
Katika muktadha wa Afrika, Tanzania imeshika nafasi ya nne, nyuma ya Botswana, Morocco na Zambia, jambo linalothibitisha ushindani wake katika kuvutia mitaji ya kimataifa katika sekta ya madini.
Ripoti hiyo pia inaonesha mwenendo chanya wa kuongezeka kwa alama za Tanzania, ambapo IAI imefikia 68.04 mwaka 2025, kutoka 62.75 mwaka 2024 na 46.38 mwaka 2023. Ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji pamoja na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji.
Kwa mujibu wa Fraser Institute, IAI hupimwa kwa kuzingatia vipengele viwili vikuu ambavyo ni uwezo wa kijiolojia wa rasilimali madini (mineral potential) na mazingira ya sera na biashara (policy framework), ambapo asilimia 60 ya uzito huwekwa kwenye rasilimali na asilimia 40 kwenye sera.
Katika kipengele cha Best Practices Mineral Potential Index, kinachoangalia uwezo wa rasilimali iwapo kungekuwa na sera bora zaidi, Tanzania imepanda hadi nafasi ya 15 duniani kwa alama 75.00, ikionyesha ukubwa wa fursa za madini zilizopo nchini.

Utafiti huo unahusisha maoni ya wataalam 2,304 wa kampuni za utafiti na uchimbaji madini, ambao kwa pamoja waliripoti kutumia takribani dola za Marekani bilioni 4.2 katika shughuli za utafiti mwaka 2025.
Matokeo haya yanaongeza msukumo kwa juhudi za Serikali kuendelea kuimarisha sekta ya madini kama nguzo muhimu ya uchumi, kwa kuongeza uwekezaji, kukuza utafiti na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini.
Wataalamu wa uchumi na wadau wa sekta hiyo wameendelea kuipongeza Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa sera na maboresho yanayochochea ukuaji wa sekta hiyo, huku wakibashiri kuwa madini yataendelea kuwa mhimili mkubwa wa uchumi wa Tanzania katika miaka ijayo.


