LONDON, Uingereza
NI miezi michache tu imebaki kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazotimua vumbi kwa mwezi mmoja kuanzia Juni, mwakani.
Kuelekea fainali hizo, baadhi ya wachezaji wako njiapanda; kuitwa au kutokuitwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba nyota hao hawapati nafasi ya kutosha ya kucheza katika klabu zao. Ni akina nani hao? Makala hayo yanachambua.
James Trafford (England)
Mlinda mlango huyo alijiunga na Manchester City wakati wa usajili uliopita wa majira ya kiangazi, mwaka huu.
Trafford alianza langoni katika mechi zote tatu za Light Kuu mwanzoni mwa msimu huu lakini kwa sasa anasugua benchi mbele ya Gianluigi Donnarumma.
Kwa hali hiyo, ni wazi itakuwa ngumu kwake kuitwa timu ya taifa ya England, ambayo tayari ina makipa Jordan Pickford na Dean Henderson.
Axel Disasi (Ufaransa)
Beki wa kati aliyekuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizopita nchini Qatar.
Kwa sasa, Disasi hapati nafasi ya kucheza pale Chelsea, hivyo amepoteza pia namba kwenye kikosi cha Ufaransa. Hajaitwa tangu mwaka 2023.
Nathan Ake (Uholanzi)
Mlinzi wa kati huyo wa kimataifa wa Uholanzi ameingia mara moja pekee katika kikosi cha kwanza cha Manchester City tangu msimu huu ulipoanza.
Kuelekea fainali zijazo za Kombe la Dunia, tayari kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi kina Virgil van Dijk, Matthijs de Ligt na Micky van de Ven katika eneo la beki wa kati.
Conor Gallagher (England)
Mwaka jana, kiungo wa kati huyo alikuwa kwenye kiwango bora akiwa na Atletico Madrid. Ni tofauti na sasa, ambapo amekuwa mchezaji wa benchi.
Msimu huu wa La Liga, Gallagher ameingia mara nne pekee katika kikosi cha kwanza cha Atletico. Ni wazi ana nafasi finyu kuitwa katika kikosi cha England kitakachokwenda Kombe la Dunia.
Kobbie Mainoo (England)
Alianza kuwika Old Trafford chini ya Erik ten Hag lakini mambo yamebadilika tangu Manchester United ilipomuajiri kocha mwingine, Ruben Amorim.
Kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika klabu yake, ni wazi Mainoo mwenye umri wa miaka 20 hawezi kumshawishi kocha wa England, Thomas Tuchel, kumwita kikosini.
Federico Chiesa (Italia)
Italia bado haijafuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani, ikisubiri mechi za ‘play-off’ zitakazochezwa Machi, mwakani.
Hata ikatokea Italia ikakata tiketi, bado Chiesa hashawishi kuitwa kwenye kikosi kitakachokwenda Kombe la Dunia. Msimu huu wa Ligi Kuu ya England, winga huyo hajaingia kikosi cha kwanza cha Liverpool.
Savinho (Brazil)
Tangu msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL) ulipoanza, Mbrazil huyo ameingia mara nne pekee katika kikosi cha kwanza cha Manchester City.
Kwa kushindwa kupata nafasi, Savinho alikaribia kuondoka Etihad wakati wa usajili uliopita wa majira ya kiangazi, mwaka huu, kabla ya kubaki na kupewa mkataba utakaokwisha mwaka 2031.
Joshua Zirkzee (Uholanzi)
Msimu huu, ameingia mara tatu pekee katika kikosi cha kwanza cha Manchester United, hivyo haonekani kuwa na nafasi ya kwenda Kombe la Dunia akiwa na Uholanzi.
Zirkzee anaweza walau kujiwekea mazingira mazuri endapo ataondoka Man United na kwenda ‘kufufua’ makali yake AC Milan, Roma, Leeds au West Ham zinazotajwa kuitaka saini yake.
Endrick
Tangu alipoajiriwa kocha Xabi Alonso, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil amecheza dakika 12 peke katika mechi za Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Hivyo, hana uhakika wa namba katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kinachonolewa na kocha Carlo Ancelotti. Ni hadi pale atakapoondoka Madrid na kwenda kurejesha makali yake katika klabu nyingine.


