Na mwandishi wetu, Gazetini
HAFLA ya droo ya hatua ya makundi tayari imeshafanyika huko Marekani, ikimaanisha sasa yangeshapatikana 12 yeye timu nne kila moja. Zilizofuzu ni 42, huku zingine sita zikisubiriwa katika mechi za ‘play-off’ hapo Machi, mwakani.
England ‘Three Lions’, kama ilivyokuwa mwaka 2018, imeangukia kundi moja na Croatia na Panama. Picha limejirudia.
England kulipa kisasi?
Mwaka 2018, wakati England ikiwa na matumaini ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 60 kupita, safari yao iliishia nusu fainali.
Safari yao ya kuingia fainali ilikwamishwa na Croatia. Kama hiyo haitoshi, England waliiokosa hata nafasi ya tatu baada ya kufungwa na Ubelgiji.
Safari hii, England watacheza mechi yao ya kwanza kwa kuivaa Croatia ifikapo Juni 17, mwakani. Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2020, England ikishinda bao 1-0, mfungaji akiwa ni Raheem Sterling.

Haaland, Mbappe nani kicheko?
Kwa miaka mingi ya hivi karibuni, mashabiki wa soka duniani kote wamekuwa wakigawanyika juu ya nani mkali kati ya Kylian Mbappe na Erling Haaland.
Hilo ni Kundi I, ambalo moja kati ya mechi zake zitazikutanisha Norway ya Haaland, dhidi ya Ufaransa yenye Mbappe.
Norway wamefuzu kwa mara ya kwanza tangu Ufaransa walipokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 1998. Ni mara ya kwanza kwa Haaland kushiriki michuano hiyo.
Messi, Ronaldo kukutana safari hii?
Kwa ufupi, haijawahi kutokea kuwaona Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakikabiliana katika michuano ya Kombe la Dunia.
Katika michuano mingine na mechi za kirafiki wakiwa na klabu na timu za taifa, mastaa hao wamekutana mara 37. Kila mmoja amefunga mabao 23, ingawa Messi ameshinda mechi nyingi (17) kuliko Ronaldo (11).
Nafasi pekee ya wawili hao kukutana Kombe la Dunia ni mwakani, ikizingatiwa kuwa wote wameshasema watastaafu baada ya hapo.
Scotland ‘kupindua meza’ kwa Brazil, Morocco?
Mara ya mwisho kwa Scotland kushiriki Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1998 na walikuwa kundi moja na Brazil na Morocco, kama ambavyo imetokea sasa (Kundi C).
Safari hii, Scotland italazimika ‘kupindua meza’ baada ya kupoteza mechi zote dhidi ya Brazil na Morocco katika fainali za mwaka 1998.
Ni wakati wa Salah kung’ara?
Licha ya kiwango chake bora akiwa na Liverpool na hata katika mechi za AFCON na za kufuzu Kombe la Dunia akiiongoza Misri, Mohamed Salah hajawahi kutikisa Kombe la Dunia.
Mwaka 2018, alishiriki Kombe la Dunia akiwa bado hajawa fiti baada ya kuumia bega katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Safari hii, Salah atakwenda Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 34 na huenda ni nafasi yake ya mwisho kwani msimu utakaofuata (2030) atakuwa na miaka 38.
Curacao kuishangaza Dunia?
Kufuzu kwa mara ya kwanza ni jambo moja. Kuwa Taifa dogo zaidi, likiwa na watu 150,000 pekee, kuwahi kufuzu Kombe la Dunia ni jambo jingine kubwa zaidi kuhusu Curacao.
Senegal, ikishiriki kwa mara ya kwanza, iliweza kuishangaza dunia kwa kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi, Ufaransa, wakati wa fainali za mwaka 2002. Ni suala la kusubiri na kuona kama Curucao nao watakuja na matokeo ya kushangaza na kuitikisa michuano hiyo.
Ujerumani watakuja kivingine?
Licha ya heshima kubwa waliyonayo katika ulimwengu wa soka, Ujerumani haijawa na mwenendo mzuri Kombe la Dunia kwa miaka ya hivi karibuni.
Kwa misimu yote miwili iliyopita, 2018 na 2022, mabingwa hao mara nne wa fainali za Kombe la Dunia waliishia hatua ya makundi.
Rekodi ya Brazil kuvunjwa?
Wenyeji wa michuano ya mwakani ni Marekani, Mexico na Canada. Kwa miaka ya hivi karibuni, mwenyeji wa michuano hiyo aliyeweza kufika mbali zaidi ni Brazil walioishia nusu fainali (2014).
Marekani imeiwekwa kundi moja na Paraguay na Australia, wakati Mexico iko na Afrika Kusini na Korea ya Kusini, huku Canada ikiwa na Qatar na Uswis.


