Na mwandishi wetu, Gazetini
KUMEKUCHA! Droo ya hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia ilichezeshwa nchini Marekani.
Kwa mara ya kwanza, fainali hizo zitashirikisha mataifa 48, huku mechi 104 zikitarajiwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali vya Marekani, Mexico na Canada.
Tukijikumbushe; timu 42 zilishakata tiketi na sasa zinasubiriwa zingine sita zitakazopatikana kupitia mechi za ‘play-off’ zitakazochezwa Machi, mwakani.
Sasa, makala haya yanaliangazia Kundi E na kuchambua timu zilizopo kuelekea michuano hiyo itakayoanza Juni 11, mwakani. Katika Kundi hili, zipo Ujerumani, Curacao, Ivory Coast na Ecuador.
Kwa misimu ya hivi karibuni, Ujerumani haijawa na maajabu, imekuwa ikiishia hatua ya makundi. Je, kocha Julian Nagelsmann atakuja na maajabu yapi?
Ecuador walifuzu wakiwa nafasi ya pili, nyuma ya Argentina, kwa upande wa mataifa ya Ukanda wa Conmebol.
Licha ya kufunga mabao 14 pekee katika mechi 18, safu yao ya ulinzi chini ya Willian Pacho (PSG) na Piero Hincapie (Arsenal) iliruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano pekee.
Ivory Coast, baada ya mafanikio makubwa ya miaka ya hivi karibuni katika michuano ya AFCON, ilifuzu Kombe la Dunia ikiwa na mabao 25 ya kufunga bila kuruhusu bao kwenye nyavu zao.
Kwa upande wao, Curacao, ambalo ndilo taifa dogo zaidi kuwahi kufuzu Kombe la Dunia, wanashiriki kwa mara ya kwanza, hivyo hata kuishia hatua ya makundi ni mafanikio makubwa kwao.


