Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu itaendelea kuisimamia na kuipa hadhi sekta ya afya ikiwemo kutoa vibali vya ajira pamoja na kujenga miundombinu ya kutolea huduma hizo katika ngazi zote.
Amesema mpango wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa uhakika na kwa usahihi, ndio maana iliamua kuwa na mkakati wa kuwapeleka Watanzania kusoma katika vyuo mbalimbali ili waje kutoa huduma kwa wananchi.
Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 5, 2025, wakati akijibu swali Mbunge wa Viti Maalumu, Jackline Andrew aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kuhakikisha wilaya zote zinapata madaktari bingwa hadi ngazi za vituo vya afya kwa ajili ya kuhudumia mama na mtoto.

Amesema ajira hizo ambazo Rais Samia anaruhusu kwa kutoa vibali kuweza kuwaajiri madaktari wakiwemo mabingwa wa magonjwa ya mama na mtoto, upasuaji ambao kwa sasa wanapelekwa hadi ngazi ya wilaya.“Tumewaagiza waganga wakuu wa mikoa kuhakikisha waangalia ikama ya madaktari bingwa na kuwapeleka kwenye maeneo yenye upungufu.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kitengo cha maafa imeweka utaratibu wa kupata taarifa za maafa yoyote kuanzia ngazi za vijiji kupitia kamati za maafa zilizoundwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.

Amesema malengo la kamati hizo ni kubaini tatizo linapojitokeza na kuharakisha kutoa taarifa katika ngazi ya juu ili kusaidia utoaji wa taarifa na kueleza ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua.
Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa ajibu swali ya mbunge wa Momba, Condester Sichwale aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali katika kukabiliana na maafa. “Kazi kubwa tunayoifanya sasa ni kuziimarisha kamati hizi kwa kuzipa elimu na mifumo inayoweza kutoa taarifa kwa haraka kwenda kamati za juu.”