21.1 C
New York

Dar yaongezwa majimbo mawili ya uchaguzi mkuu

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) imeanzisha majimbo mapya nane ya uchaguzi na kubadilisha majina ya majimbo 12 ambapo Mkoa wa  Dar es Salaam yameongezwa majimbo mawili la Kivule na Chamazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Mei 12, 2025 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mamlaka ya tume katika kurekebisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi nchini.

Ameyataja majimbo mengine  yaliyoanzishwa kuwa  ni mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya ya uchaguzi la Mtumba baada ya Dodoma mjini kugawanywa. Mkoani Mbeya limeanzishwa Jimbo jipya moja la Uyole ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa.

Ameeleza  kuwa mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Bariadi Mjini wakati  mkoani Geita yameanzishwa majimbo mawili ambapo Jimbo la Uchaguzi la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Katoro na Jimbo la Uchaguzi la Chato limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Chato Kusini.

“Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi,” amesema Jaji Mwambegele.

Kuhusu majimbo 12 yaliyobadilishwa majina ameyataja kuwa ni Jimbo la Uchaguzi la Chato ambalo limebadilishwa jina kuwa Chato Kaskazini.

“Jimbo la Uchaguzi la Nkenge limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Missenyi, Jimbo la Uchaguzi la Mpanda Vijijini limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Tanganyika na Jimbo la Uchaguzi la Buyungu limebadilishwa jina sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Kakonko,” ameeleza.

Ameongeza kuwa Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Bariadi Vijijini, Jimbo la Uchaguzi la Manyoni Mashariki limebadilishwa jina na kuwa Jimbo la Uchaguzi la Manyoni na Jimbo la Uchaguzi la Singida Kaskazini limebadilishwa jina na kuwa Jimbo la Uchaguzi la Ilongero.

Majimbo mengine ni Jimbo la Manyoni Magharibi kuwa Jimbo la Itigi, Jimbo la Singida Mashariki kuwa Jimbo la Ikungi Mashariki, Jimbo la Singida Magharibi kuwa Jimbo la Ikungi Magharibi, Jimbo la Tabora Kaskazini kuwa Jimbo la Uyui na Jimbo la Handeni Vijijini kuwa Jimbo la Handeni.

Amefafanua kuwa kutokana na ongezeko hilo, idadi ya majimbo kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika  Oktoba 2025 yatakuwa 272  ambapo 222 yakiwa Tanzania Bara huku 50 yakiwa Zanzibar.

Aidha ameeleza kuwa kutakuwa na kata 3,960 zitakazofanya uchaguzi wa madiwani kwa Tanzania Bara katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img