Na Jackline Jerome, Gazetini
Tanzania inaongoza barani Afrika na duniani kwa ujumla kwa kuwa na idadi kubwa ya simba, ikiwa na jumla ya takribani simba 17,000, wengi wao wakiwa katika ikolojia za Serengeti na Selous, kwa mujibu wa taarifa za IUCN (2023) na Ripoti ya Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori na mazingira duniani (WWF). Afrika Kusini inafuata kwa kuwa na simba 3,300, ikiwemo 3,284 walioko Hifadhi ya Kruger, na Botswana ikiwa na simba 3,064 wanaopatikana zaidi katika Delta ya Okavango.
Hadi karne ya 20, zaidi ya simba 200,000 walikuwa wakizurura katika mabara ya Afrika, Asia na Ulaya, lakini idadi hiyo sasa imepungua hadi chini ya simba 20,000 duniani — sawa na upotevu wa asilimia 90, kutokana na ujangili, kupotea kwa makazi yao na migogoro baina ya binadamu na wanyama.
India ina simba 680 pekee wa Asia walioko kwenye Msitu wa Gir, huku Kenya ikiwa na simba 2,515 wanaopatikana hasa Maasai Mara.