1.7 C
New York

Chart| Maambukizi ya VVU kwa vijana wanaojiunga JKT

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Februari 3, 2023 Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliwasilisha taarifa yake bungeni kwa kipindi cha Februari 2022 hadi Februari 2023 na kueleza kuwa vijana 147 kati ya 67,299 waliojiunga JKT kwa mujibu wa sheria walikutwa na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI(VVU).

Sehemu ya taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu, yaani kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2021, Jeshi la Kujenga Taifa limechukua vijana kwa mujibu wa sheria ambapo Mwaka 2019 vijana 20,413; Mwaka 2020 vijana 21,383 na Mwaka 2021 vijana 25,503.

“Hali ya maambukizi kwa vijana waliokuwa Makambini kwa mujibu wa sheria kwa miaka hiyo mitatu ni kama ifuatavyo: Mwaka 2019 kati ya vijana 20,413 waliopimwa vijana 60 walikutwa na maambuzi; mwaka 2020 kati ya vijana 21,383 waliopimwa vijana 45 walikutwa na maambukizi na mwaka 2021 kati ya vijana 25,503 waliopimwa vijana 42 walikutwa na maambukizi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa:

“Vijana wenye Virusi vya UKIMWI katika Jeshi la Kujenga Taifa wanapatiwa huduma mbalimbali kama vile ushauri nasaha kabla ya kupimwa VVU; Kupatiwa/kuanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV).

“Kupatiwa vipimo muhimu kabla ya kuanza dawa na hata baada ya kuanza dawa vipimo kama vya figo, maini na CD4 Count na Viral load (Wingi wa virusi kwenye damu) pamoja na kupimwa magonjwa nyemelezi kama Kifua Kikuu, Homa ya Uti wa mgongo ya fungus na kutibiwa magonjwa nyemelezi endapo watakutwa nayo,” ilieleza taarifa hiyo ya Kamati.

Aidha, kamati hiyo ilieleza kwamba imebaini kuwa bado elimu kuhusu umuhimu wa kujua afya ni mdogo lakini pia fedha za utekelezaji wa afua hazitoshelezi mahitaji.

“Kamati inaona kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kupima na namna ya kujikinga na maambukizi mapya kwa vijana,” imeeleza taarifa hiyo.

JKT imesema nini

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 6, 2023, Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema taarifa zilizotolewa na kamati ni sahihi.

“Vijana ambao hukutwa na changamoto ya kiafya hufanya mafunzo yao chini ya uangalizi wa wakufunzi ili kuhakikisha wanamaliza mafunzo yao salama,” amesema.

Wanavyopatikana Vijana wa JKT

Kulingana na utaratibu uliowekwa Jeshi la Kujenga Taifa hupokea Vijana ambao wamehitimu kidato cha sita.

Vijana hao huripoti Makambini kwa ajili ya mafunzo bila kujali hali ya afya zao, wote hujumuishwa kuhudhuria mafunzo hayo, ingawa kabla ya kuanza mafunzo wote hulazimika kupimwa afya zao, wale ambao watagundulika kuwa wajawazito tu ndio hurejeshwa nyumbani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img