7.9 C
New York

Utafiti| Wanafunzi ‘wamesahaulika’ mapambano ya VVU

Published:

*Serikali inakumbushwa kuchukua hatua ikiwamo kubadili sera
*Wazazi nao watakiwa kutokubaki nyuma

Na Faraja Masinde, Gazetini

Ni zaidi ya miaka 40 sasa imepita tangu janga la Virusi Vya UKIMWI lilipoanza kuitikisa dunia.
Tanzania kama sehemu ya nchi zinazounda ukamilifu huo inaendelea na mikakati ya kila namna katika kuhakikisha kuwa inadhibiti UKIMWI ifikapo 2030.

Hata hivyo, sambamba na Tanzania kuonyesha dalili njema katika kudhibiti janga hilo, ni bayana kwamba bado kuna kazi ya ziada inapaswa kufanyika ili juhudi hizo za Serikali na wadau ziweze kuleta manufaa.

Ifahamike kuwa kwasasa Tanzania ina jumla ya watu milioni 1.7 wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.

Kati ya watu hao, 99,000 ni vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 19 ambao kwa umri huo wengi bado wako shuleni na wanahitaji msaada katika mazingira ya shule pamoja na kliniki rafiki za VVU.

Aidha, katika vijana hao 99,000 kati yao 57,000 ni vijana wa kike huku waliobaki wakiwa wakiume.
Takwimu hizo zinakuja katika wakati ambao tunaelezwa kuwa nusu ya maambukizi mapya ya VVU duniani kote yalitokea kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24.

Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu-(NIMR) umebaini kuwa vijana wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI(ALHIV) wameachwa bila msaada hususan maeneo wanayotumia muda wao mwingi ambayo ni shule na vyuo.

Changamoto hizo ni pamoja na kukosa huduma rafiki za VVU, unyanyapaa na ubaguzi, ukosefu wa msaada kutoka kwa wazazi/walezi na walimu, ukosefu wa huduma za matunzo ya VVU, ufichuzi, umbali na umaskini.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo katika kikao kilichojumhisha wadau mbalimbali wakiwamo wa Wizara zinazohusika ambazo ni Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na wadau wengine muhimu.

Dk. Andrew Kigombola ni Mshauri Mwelekezi na mmoja wa washiriki wa utafiti huo uliofanyika mwaka 2021, ambapo akiwasilisha matokeo hayo hivi karibuni jijini Dodoma, anasema kuwa wamebaini changamoto nyingi ambazo Serikali na wadau wanapaswa kuzitatua ili kuleta ustawi kwa watoto hao na kusaidia mapambano ya VVU.

Akizungumza kuhusu Wizara ya Elimu Dk. Andrew anasema kuwa ili kuhakikisha uratibu wenye ufanisi, mapitio ya miundo ya uratibu yanapaswa kufanywa kwa mwelekeo wa maafisa juu ya majukumu na wajibu kuhusu utekelezaji wa programu ya afya shuleni na afua za VVU.

Kamu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS,. Jumanne Issango akifungua Mdahalo wa wadau wa Utekelezaji wa Shughuli za UKIMWI na uboreshaji wa utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI shuleni. Mdahalo huo uliofanyika Oktoba, mwaka huu jijini Dodoma ukihusisha Wizara, Vijana na Wawakilishi wa Baraza la watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI(NACOPHA).

Anasema maambukizi ya VVU hayapaswi kuachwa nyuma shuleni na kwamba wanafunzi wanapaswa kujengewa uwezo juu ya jambo hilo.

“Kamati ya Ushauri ya Kiufundi shuleni zinapaswa kuratibu na kuwajibika kwa afua zote za afya shuleni ikijumuisha VVU.

“Hii itasaidia kuhakikisha utekelezaji mzuri wa shughuli za afua za VVU katika mazingira ya shule. Sambamba na hayo serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele kwa kuweka msukumo wa ufadhili ili kukidhi mahitaji ya vijana wawapo shuleni.

“Bajeti hii pia inapaswa kufika hadi ngazi ya Halmashauri ili kuweza kusaidia wadau waliko katika nyanja ya kutoa elimu ya uzazi na jinsia pamoja na shughuli za VVU kwa vijana, hivyo iwapo wizara hizi zitashirikiana kikamilifu itasaidia vijana kuweza kufikiwa na huduma na kuondoa dhana ya kunyanyapaliwa hatua mbayo imekuwa ikidhorotesha ufuasi wa dawa kwa vijana wengi,” anasema Dk. Andrew.

Anasema shule zinapaswa kuwa na wahudumu wa afya wenye ufanisi mkubwa watakao kuwa na msaada kwa vijana wanaoishi na VVU ili waweze kupata huduma wawpo shuleni pindi inapohitajika kufanyika hivyo.

“Kimsingi jambo hili linapaswa kuratibiwa na Wizara ya Elimu, likienda pamoja na kujengewa uwezo walimu kupitia mafunzo rasmi na ushauri katika elimu ya uzazi na jinsia itakayosaidia vijana wanaoishi na VVU ili kuhakikisha wana ujuzi muhimu katika ushauri nasaha na usimamizi,” anasema Dk. Andrew.

Dk. Edward Machage Naibu Mkuu wa Kitengo cha afua za tiba na matunzo ya VVU kutoka CDC akichangia mada ya kuzuia na kuboresha huduma za afua za UKIMWI shuleni katika Mdahalo wa wadau wa utekelezaji wa shughuli za UKIMWI, Wizara, Vijana na wawakilishi wa Baraza la watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kuhusu uboreshaji wa utoji wa huduma za VVU na UKIMWI shuleni.

Anafafanua zaidi kuwa kunapaswa kuwapo na utaratibu wa shule kuratibu taarifa zitakazoandaliwa ili kunasa hafua zote za afya shuleni ikiwa ni pamoja na huduma za VVU.

Mkazo Wizara ya Afya

Dk. Andrew anasema kuwa Wizara ya Afya ambayo ndiyo mama katika nyanja ya afya, inapaswa kuandaa na kusambaza mwongozo maalum au waraka kwa ajili ya utoaji wa huduma za VVU katika mazingira ya shule nchini.

“Ukiangalia katika sehemu tulizofanya utafiti bado hakuna mazingira rafiki kwa mwanafunzi mwenye VVU kuweza kutoa taarifa, hivyo ni jukumu la wizara kuja na waraka ambao utakuwa na msaada katika hili.

“Hii pia itaelekeza uongozi wa shule na walimu jinsi ya kusaidia Vijana Wanaoishi na VVU, kushughulikia unyanyapaa na ubaguzi, msaada wa uteuzi na ufuasi wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi(ARVs),” anasema Dk. Andrew.

Kuhusu wizara ya TAMISEMI, utafiti huo umebainisha kuwa mikoa inapaswa kuteua na kupata waratibu wa afya shuleni.

“Uratibu na ushirikiano kati ya idara hizo mbili unapaswa kuimarishwa na kuungwa mkono chini ya uongozi wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili shughuli za kusaidia afua za afya shuleni ikiwa ni pamoja na kusaidia vijana wanaoishi na VVU zifanyike mara kwa mara.

“Aidha, ili kuhakikisha utoaji wa afua bora za afya na huduma za VVU katika mazingira ya shule, waratibu wa ngazi ndogo za kitaifa wanapaswa kuwezeshwa kwa ziara za mara kwa mara shuleni kwa ajili ya ukaguzi wa ubora, usimamizi, ushauri na shughuli za kujenga uwezo kwa wahusika,” anasema.

Kwa mujibu wa Mtaalamu huyo, hadi sasa ni walimu takribani 2,000 tu nchi nzima ndiyo wamejengewa uwezo juu ya huduma za VVU kiwango ambacho hakitoshi ikilinganishwa na idadi ya shule zilizopo nchini.

“Ni kweli kwamba kila mkoa kuna waratibu wa huduma za VVU lakini ukweli ni kwamba kufika shuleni bado ni changamoto na ndiyo sabahu tunahitaji kutumia wadau waliko katika maeneo ya mikoa yetu kuweka msukumo wa uwezeshwaji ili shule ziweze kuwa na watu wa namna hii au kujengewa uwezo ikiwamo vijana wenyewe,” anasema Dk. Andrew na kuongeza kuwa kuna haja ya kuongeza ushirikiano baina ya wizara zote husika.

Anasema kwa kufanya hivyo kutatekeleza na kuratibu huduma za afya shuleni ikiwamo kuwajengea uwezo kupitia mafunzo waalimu na waratibu katika kutoa huduma za afya na kutengeneza muongozo wa rufaa na ushirikiano kati ya shule na vituo vya afya ili kutoa huduma za afya shuleni.

Utafiti huo unabainisha kuwa ili kusaidia zaidi afua za VVU katika mazingira ya shule, washikadau kama vile washirika wa utekelezaji (IPs) na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UNESCO na UNICEF) wanapaswa kutoa usaidizi wa kifedha.

“Pia uratibu wa mikutano ya programu ya afya ya shule na afua za VVU shuleni kupitia Kamati ya Ushauri ya Kiufundi,” anasema Dk. Andrew.

Naibu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Scholastica William akielezea umuhimu wa Baraza hilo katika uratibu wa WAVIU na hafua a afafua za VVU na UKIMWI nchini.

Upande wa wazazi na walezi ambapo unabainisha kuwa ili vijana wanaoishi na VVU waweze kupata huduma bora shuleni, basi hali yao ya VVU inapaswa kuwekwa wazi kwa walimu wa afya.

“Wazazi na shule washirikiane ili kuwasaidia watoto wao ikiwamo kubainisha hali zao za VVU, hii itawawezesha kupata huduma na usaidizi unaohitajika.

“Upande wa shule, Mwalimu Mkuu na kamati ya afya wahakikishe angalau mwalimu mmoja wa afya anapatikana ili kusaidia vijana wanaoishi na VVU na watoto wengine wenye mahitaji ya afya.

“Pia, kuendeleza na kukuza uhusiano na vituo vya afya ili kuhakikisha vijana wanaoishi na VVU wanasaidiwa kuzingatia dawa zao na kuhakikisha uhifadhi bora wa dawa katika mazingira ya shule,” anasema na kuongeza kuwa:

“Kwa usaidizi wa walimu wa afya, vijana wanaoishi na VVU wanapaswa kuruhusiwa kuhudhuria kliniki za CTC kwa ajili ya kujazwa tena dawa na ukaguzi wa afya.

“Kupitia ushirikiano na wazazi na ridhaa zao, vijana wanaoishi na VVU wanapaswa kuhimizwa kufichua hali zao kwa mwalimu wa afya aliyeteuliwa ili waweze kusaidiwa wakati wa shule.

“Kama sehemu ya mpango wa chakula shuleni, watoto wanaokwenda shule ikiwa ni pamoja na vijana wanaoishi na VVU wanapaswa kusaidiwa kupata milo yenye lishe bora kwa kutumia bajeti kamili ya halmashauri. Kutumia programu zingine zinazosaidia lishe kunahimizwa,” anabainisha Dk. Andrew kupitia ripoti hiyo na kuhitimisha kuwa:

“Waratibu katika ngazi ya chini na walimu wakuu wanapaswa kuhakikisha shule zote zina vilabu vya wenzao wa afya na kuwashirikisha vijana wanaoishi na VVU katika vilabu hivi ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza moja kwa moja uzoefu wa vijana wanaoishi na VVU katika jinsi ya kukabiliana na unyanyapaa,”.

Upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uragabishi kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS), Jumanne Issango akizungumzia utafiti huo anasema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa kundi hilo la vijana kupata huduma za VVU wawapo shuleni.

“Vijana wanahitaji kusaidiwa ili waweze kujikwamua na changamoto hizi, sababu bado wako kwenye uangalizi na maandalizi ili waweze kufika mahala ambapo watasaidia kutoa mchango wao katika ustawi wa Taifa letu,” anasema Issango.

Upande wake Naibu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Scholastica William anasema kuwa watoto na vijana balehe ni moja ya makundi wanayoyatazama katika kutatua changamoto zao.

“Tunashukuru kama NACOPHA kuona ni kwanamna gani tunashirikishwa katika kuleta changamoto zetu juu ya wapi penye upungufu katika kufikia malengo ikiwamo yale ya kisera, hivyo kwa namna ambavyo muda unazidi kwenda ndiyo tumekuwa tukipewa nafasi, hivyo ni imani yetu kuwa mawazo yetu yatafanyiwa kazi na kuja na mkakati bora ambao utasaidia makundi yote ya waviu wakiwamo vijana waliko shule,” anasema Scholastica.

John George ambaye ni Mkuu wa Idara ya VVU na UKIMWI kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) anabainisha kuwa vijana wanaoishi na VVU ambao wako shuleni wanakabiliwa na changamoto ikiwamo ya ukosefu wa elimu, unyanyapaa na kukosa muda wa kwenda kuchukua dawa.

“Unyanyapaa huu umesababisha baadhi ya vijana kutokuweka hali zao wazi na ndiyo sababu tunaambiwa kuwa vijana ambao wananzia miaka 15 hadi 19 ufuasi wao wa dawa uko chini ikilinganishwa na wale wenye umri wa miaka 10 hadi 14 kwani wako chini ya himaya ya wazazi.

“Jambo jingine ni mfumo wa vijana walioko shuleni ambao wanalazimika kuomba ruhusa ili kwenda kufuata dawa zilipo jambo ambalo limekuwa ni changamoto, hivyo kama wadau tuna kazi ya kufanya katika kuhakikisha kuwa huduma zinafika shuleni,” anasema George.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img