LAGOS, Nigeria
MKONGWE wa timu ya soka ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’, Austin Jay-Jay Okocha, ameeleza kushangazwa na kiwango kizuri alichonacho mtoto wa dada yake, Alex Iwobi.
Iwobi amekuwa mchezaji muhimu si tu kwa Eagles, bali pia kwa klabu yake ya Fulham inayoshiriki Ligi Kuu ya England [EPL].
Okocha amekiri kuvutiwa na maendeleo ya soka aliyonayo mpwa wake huyo, akidai kuwa hakuwahi kutarajia kumuona akicheza kwa kiwango alichonacho sasa. “Amenishangaza,” amesema Okocha.
Kubwa zaidi, Okocha aliyewahi kuzitumikia Bolton na PSG kwa nyakati tofauti, amesema anajisikia fahari kuona Iwobi amevuka idadi ya mechi zake alizowahi kuitumikia Eagles.
Takwimu zinaonesha kuwa Iwobi ameshacheza mechi 104 akiwa na Eagles, akimpiku Okocha aliyestaafu akiwa ametumika mara 73 katika kikosi hicho.
Aidha, Iwobi anaendelea kuwa mmoja ya wachezaji watano pekee waliocheza mechi walau 100 wakiwa na Eagles. Wengine ni Ahmed Musa, Vincent Enyeama, Joseph Yobo na Moses Simon.


