Na mwandishi wetu, Gazetini – KILIMANJARO
WAKATI shule nyingi zikiendelea kupokea wanafunzi wapya kwa mwaka wa masomo 2026-27, Shule ya Msingi Jipe iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, imekumbwa na uhaba wa wanafunzi, hali iliyowafanya wazee wa kijiji hicho kuwatupia lawama vijana kwa kushindwa kuoa na kuanzisha familia.
Hali hiyo imeibua hofu kuhusu mustakabali wa shule hiyo baada ya wanafunzi wawili pekee, ambao ni ndugu, kuhitimu darasa la saba mwaka huu, huku shule nzima ikiwa na wanafunzi 79 kuanzia darasa la awali hadi la saba.
Wakazi wa kijiji hicho wanasema vijana wengi wamekuwa wakihamia mijini kutafuta maisha na wengine kukwepa kuoa kwa madai ya ugumu wa maisha.
Mwalimu mstaafu wa Shule hiyo, Mussa Mziray, amesema idadi ya wanafunzi imeendelea kupungua, ikilinganishwa na kipindi alichokuwa akifundisha, akieleza kuwa vijana wengi wanaohamia mijini huanzisha familia huko na kuwaacha wazee kijijini.
Naye Naseeb Mziray, babu wa wahitimu hao, amesema hali hiyo inashangaza na kuwataka vijana kuoa ili kuendeleza kizazi kijijini hapo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Khatibu Mziray, amesema shule hiyo iko hatarini kukosa wanafunzi wa kuendelea na masomo endapo hali hiyo haitabadilika.
Hata hivyo, mwalimu wa shule hiyo, Elidaima Mkwizu, amesema wanafunzi 15 walianza darasa la kwanza, lakini idadi ilipungua kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uhamisho wa baadhi ya watoto kwenda shule nyingine.
Diwani wa kata hiyo, Hussein Mfangavo, amesema wamepanga kufanya kikao Desemba, mwaka huu, kujadili changamoto hiyo na kutafuta suluhisho.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amethibitisha kuwa wanafunzi wawili walihitimu darasa la saba katika shule hiyo, akieleza kuwa sababu nyingine ni mazingira ya kiuchumi yanayosababisha wakazi wengi kuingia na kutoka katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, amesema Mkoa una shule za msingi 1,000 ambazo wanafunzi 35,654 wamehitimu darasa la saba mwaka huu.


