18.2 C
New York

Wajasiriamali Tanzania waitiwa fursa Rwanda

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

BALOZI wa Tanzania nchini Rwanda, Dkt. Habib Gallus Kambanga, ameahidi kuwatafutia fursa za masoko wajasiriamali wa Tanzania ili kuuza bidhaa zao, kupanua wigo wa biashara na kuongeza kipato.

Amesema hayo katika mazungumzo yake na ujumbe wa Tanzania uliofika ubalozini jana Novemba 4, 2026, kwa ajili ya kujitambulisha na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maarufu ‘Nguvu Kazi au Jua Kali’, yanayoendelea mjini Kigali.

Balozi Kambanga ameeleza kuwa ubalozi huo utaendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wajasiriamali wa Tanzania na wanunuzi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa biashara nchini Rwanda.

“Nitoe wito kwa wajasiriamali kuendelea kutumia fursa zinazotokana na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Rwanda kwa kuimarisha ushirikiano katika uzalishaji, biashara na uwekezaji,” amesema.

Wakati huo huo, Balozi Kambanga amepongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha wajasiriamali kushiriki katika maonesho hayo.

Maonesho hayo ya Jua Kali yanaongozwa na Kaulimbiu ‘Kuendeleza mnyororo wa thamani katika Sekta ya Ngozi na Kilimo cha Bustani katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki’ yalianza Oktoba 30 yakitarajiwa kufikia ukomo Novemba 9, 2026.

Related articles

Recent articles