Na Hassan Mwasha, Gazetini
HIVI karibuni, lilikuwepo tishio la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA], Tundu Lissu, kugome chakula na kutokutumia dawa akiwa gerezani.
Hatua hiyo ililenga kuwasilisha hisia zake baada ya uongozi wa Gereza la Ukonga kutotekeleza agizo la Mahakama Kuu linalomruhusu kukutana na mawakili wake kwa faragha.
Oktoba 27, 2026, Lissu alisusia chai asubuhi kwa kuwa makubaliano ya awali ya kuonana na mawakili wake kwa faragha yalikuwa bado hayajatekelezwa kikamilifu.
Hata hivyo, uongozi wa magereza uliruhusu mawakili wake, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, kuzungumza naye kwa faragha kwa takribani saa mbili. Baada ya haki hiyo kutimizwa, Lissu alisitisha mgomo huo rasmi.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa walioko kizuizini kuchukua hatua hiyo kama njia ya kufikisha hasira zao kwa mamlaka za gereza na Serikali kwa ujumla. Makala haya yanachambua.
KIZZA BESIGYE [UGANDA]
Februari 11, 2026, mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Uganda aliweka mgomo wa kula akipinga Mahakama ya kijeshi kusikiliza kesi yake ya uhaini.
Besigye [68], ambaye amewahi kuwa daktari binafsi wa Rais Yoweri Museveni, alisitisha mgomo huo baada ya Mahakama ya kijeshi kujiweka kando na Mahakama ya kiraia kuanza kusikiliza kesi yake.
SUCCES MASRA [CHAD]
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Chad na sasa ni kiongozi wa siasa za upinzani nchini humo. Juni 30, 2025, Masra aligoma kula kwa wiki moja akiwa kizuizini kwa mashitaka mbalimbali, ikiwamo kushirikiana na magenge ya uhalifu.
Masra Alisitisha mgomo Julai 1, 2025, baada ya kushauriwa na madaktari wake. Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 [Agosti, 2025], kabla ya kutolewa kwa msamaha wa Rais Mahamat Idriss Deby miezi michache iliyopita.
ABIR MOUSSI
Huyo ni kiongozi wa Chama cha upinzani nchini Tunisia, Free Constitutional Party (PDL). Amegomea kula mara kadhaa tangu alipoingia gerezani Oktoba, 2023.
Januari, 2024, aligomea kula na kunywa maji kwa siku mbili akilalamikia hali mbaya ya mazingira katika gereza analoishi. Alilalamikia pia kunyimwa haki ya familia yake kumtembelea.
MAHATMA GANDHI
Kiongozi wa harakati za uhuru wa Taifa la India. Katika maisha yake ya siasa, aliwahi kugomea kula mara 18 kwa nyakati tofauti.
Mfano, aliwahi kugomea kwa siku 21 [Septemba 18 – Oktoba 8, 1924). Pia, aliwahi kugoma kula kwa siku sita [Septemba 20–26, 1932) akiwa kizuizini kwenye gereza la Yerwada.


