4 C
New York

Joseph Kabila mzalendo au muasi wa DRC?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

JOSEPH Kabila ndiye aliyekuwa kamanda wa kikosi wakati muungano wa waasi ulipopindua Serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo [DRC] na kumuweka madarakani baba yake mzazi mwaka 1997.

Baadaye, Kabila akawa rais akichukua nafasi ya baba yake na sasa akiwa na umri wa miaka 55, miaka 18 tangu alipoondoka madarakani, amerudi tena kwenye kiti cha kiongozi wa waasi kujaribu kumng’oa Ikulu Rais Felix Tshisekedi.

Ndiyo, Kabila katika nafasi yake ya Rais Mstaafu, ameamua amejiunga na kuwa kiongozi wa Front for the Refoundation of the Nation (FRN), moja ya makundi ya waasi yanayoupinga kwa nguvu zote utawala wa Rais huyo.

UADUI ULIANZIA WAPI?

Kama itakumbukwa, Kabila alifanya jitihada kubwa kuhakikisha Tshisekedi ndiye anayechukua nafasi yake kwenye kiti cha urais badala ya Martin Fayulu, ambaye Kanisa Katoliki nchini humo lilimtaja kuwa ndiye aliyeshinda katika Uchaguzi wa mwaka 2018.

Hata aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Corneille Nangaa, amewahi kukiri kuwa Kabila na Tshisekedi walikaa mezani na kusuka mpango wa kumpora ushindi mgombea huyo [Fayulu]. “Naweza kuthibitisha kuwa nilihusika katika mpango huo,” alisema Nangaa alipohojiwa na kituo cha habari cha France 24 mwaka 2023.

Licha ya Tshisekedi kukanusha na kusema alishinda kwa kura halali za wananchi, Nangaa aliongeza: “Tshisekedi ni muongo. Anafahamu wazi kuwa yalikuwapo makubaliano na anajua kilichokubaliwa kwenye makubaliano hayo.”

Katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni makubaliano ya mezani waliyoingia kabla ya Uchaguzi, hata baada ya Rais Tshisekedi kuingia Ikulu, wanasiasa wa Kabila waliendelea kutawala bungeni.

Upepo ulibadilika ghafla baada ya kile alichokifanya Tshisekedi mwaka 2020, ambapo aliwabwaga vigogo wengi wa Kabila na kuteua wengine waliokuwa upande wake. Uadui uliaanzia hapo na ndipo Kabila akaanza kusikika hadharani akiikosoa Serikali.

MZALENDO AU MUASI?

Baada ya Kabila kutangazwa kuwa kiongozi mpya wa FRN mwezi uliopita, Tshisekedi alisema: “Kwa mtazamo wangu, ni ushahidi tosha kuwa hajawahi kuipenda nchi hii na watu wake.”

Kujiunga na FRN kunathibitisha madai ya muda mrefu ya wakosoaji wa Kabila waliokuwa wakidai kuwa kiongozi huyo anashirikiana kwa siri na waasi kuiyumbisha Serikali iliyoko madarakani. Alitajwa kushirikiana na M23.

M23 ni kundi kubwa zaidi miongoni mwa yaliyopo sasa, ambalo mwaka jana liliteka sehemu kubwa ya Mashariki mwa DRC, ikiwamo miji muhimu ya Goma na Bukavu.

Baada ya kurejea DRC mwaka 2025, Kabila alionekana Goma, Mji unaoshikiliwa na waasi hao. Miezi michache tu baadaye, mahakama ilimuhukumu kifo kwa mashitaka ya uhaini.

Pia, kile kilichoonekana kuwa ni uasi wa wazi ni ukaribu wake na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye kwa miaka mingi DRC na jumuhiya za kimataifa zimekuwa zikiitaja serikali yake kushirikiana na M23.

Kwa wachambuzi walio wengi, hatua ya sasa ya Kabila kujiunga na waasi ni sehemu ya njia zake za kutaka kurejea kwenye ushawishi wa siasa kwenye Taifa hilo lenye utajiri wa rasilimali nyingi, hasa madini.

Je, ni rahisi kiasi gani kwa Kabila kumtoa Tshisekedi? Hilo linajibiwa na mchambuzi wa siasa kutoka Taasisi ya Maafa ya Crisis Group, Richard Moncrieff, akisema bado kuna kazi kubwa inayomkabili Rais huyo wa zamani.

“Tshisekedi anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Marekani. Ana pesa nyingi na ndiye anayedhibiti mfumo wa siasa na jeshi kama tunavyoweza kuona,” amesema Moncrieff.

Related articles

Recent articles